Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela ameongoza makubaliano baina ya Wakulima wa miwa katika bonde la Kilombero na Kiwanda cha Sukari cha Kilombero yenye lengo la kutatua changamoto mbalimbali zilizojitokeza baina ya pande hizo mbili.
Akizungumza hivi karibuni mara baada ya Kikao cha majumuisho kilichodumu kwa zaidi ya masaa 10 kati ya Uongozi wa Kiwanda hicho na Viongozi wa vyama vya wakulima wa miwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero na Kilosa, Shigela amesema yapo makubaliano mengi yaliyofikiwa kati ya pande hizo mbili ambazo zinatarajiwa kuleta tija kwa wakulima pasipo kuathiri uendeshaji wa Kiwanda.
Miongoni mwa makubaliano yaliyofikiwa ni pamoja na kila Mkulima kuwa na namba yake binafsi ya utambulisho itakayomwezesha apate malipo stahiki kulingana na kiasi cha miwa alichozalisha badala ya namba ya Mkulima mmoja kutumika na mkulima zaidi ya mmoja.
“Katika kilimo cha miwa ambacho Mkoa wetu ndio kinara, zipo changamoto zilizokuwa zikiwakabili wakulima wetu ikiwemo baadhi ya wakulima kutokuwa na namba ya utambulisho, tumekubaliana kwamba kila Mkulima atauza miwa kwa kutumia namba yake ya utambulisho na pesa italipwa katika akaunti yake mwenyewe”
Aidha Shigela amebainisha kuwa jambo lingine lililoafikiwa baina ya pande hizo mbili ni kuwepo uwakilishi wa wakulima katika kupima kiwango cha thamani ya sukari iliyotokana na miwa ya Mkulima badala ya kiwango hicho kufahamika baada ya malipo.
Mbali na hayo Mkuu huyo wa Mkoa amesema Uongozi wa Kiwanda cha Sukari cha Kilombero na Wakulima wa Miwa wameafikiana kwamba Mkandarasi atakayetupa miwa kutokana na kuzidisha uzito wa mzigo wa miwa kwenye gari lake huku akifahamu uzito unaohitajika kuingia kiwandani atawajibika kulipa miwa hiyo kwa pesa zake binafsi.
Shigela amewataka Wakandarasi wanaohusika kubeba miwa ya Wakulima kutoka shambani kuhakikisha wanabeba kulingana na uwezo wa magari yao na kuzingatia kiwango cha uzito kinachohitajika Kiwandani.
Hata hivyo Shigela amewahakikishia Wakulima wa miwa kwamba Serikali itashughulikia changamoto zinazowakabili katika shughuli zao za Kilimo cha miwa ikiwemo masuala ya Pembejeo huku akiupongeza Uongozi wa Kiwanda hicho, Viongozi wa Vyama vya Wakulima wa miwa Pamoja na Wakulima wa zao hilo kwa kukubali kukaa Pamoja na kumaliza changamoto zilizojitokeza.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya mahusiano wa Kiwanda hicho Efraim Mafuru amemuhakikishia Mkuu wa Mkoa na wakulima wote wa miwa kwamba watayatekeleza makubaliano yote yaliyofikiwa ili kufanikisha ukuaji na uzalishaji wa Kiwanda hicho.
Naye Mwenyekiti wa vyama vya Wakulima wa miwa Bakari Mkangamo amemshuru Mkuu wa Mkoa na Serikali kwa jumla kwa kufika na kusikiliza changamoto zilizojitokeza na kutumia muda wake wa siku tatu kutatua kero hizo na kuahidi kuongeza uzalishaji wa miwa kupitia wakulima waliopo.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.