Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela ametoa karipio kwa madalali wa zao la miwa wasio waaminifu hivyo kutumia nafasi zao na kuwadhulumu wakulima wa zao la Miwa wa Wilaya za Kilombero na Kilosa Mkoani Morogoro.
Shigela ametoa karipio hilo Mei 12 Mwaka huu katika ziara yake ya kutatua Kero za wananchi hususan wa Kikundi cha AMCOS cha wakulima wa miwa wa Kijiji cha Sanje Kata ya Sanje Wilayani Kilosa Mkoani humo.
Mkuu huyo wa Mkoa amebainisha kuwa Madalali ya kusaidia wakukima wao wamekuwa chanzo cha wakulima kupoteza haki zao za msingi ikiwemo kutonufaika vema na zao hilo la Muwa, ambapo ametaka kuondoshwa madalali hao ili wananchi waweze kunufaika na zao hilo kwa kujiletea maendeleo yao.
“Wapo Madalali hawana mashamba ya Miwa lakini kila Mwaka ni wauzaji wa Miwa pale. Mwaka huu hakuna hata mtu mmoja atakayeuza Miwa asiyekuwa na shamba, wale mliojipanga kufanya hivyo mkatafute biashara nyingine ya kufanya vinginevyo mtaenda kuozea jela na hili namaanisha.." amesema Shigela.
Katika hatua nyingine Martine Shigela ameoneshwa kukerwa na makato mbalimbali ya tozo zilizo nje ya mkataba wa uvunaji wa Miwa ambazo zimekuwa mzigo mzito kwa wakulima na kusababisha wakulima hao kuendelea kuwa masikini.
Akisoma masharti na vigezo vya kumpata Mkandarasi wa Uvunaji wa Miwa Bwana Jackson Mushumba ambaye ni Afisa Ushirika wa Kanda Bonde la Kilombero amesema, mojawapo ya Masharti hayo ni Mkandarasi kuwa na magari yaliyo bora kiutendaji kwa ajili ya kusafirisha Miwa, AMCOS zilizo na DRD kuanzia 150 zinatakiwa kuajili wakandarasi wawili na mkandarasi awe tayari kukatwa kwenye malipo yake ili kufidia hasara atakazosababisha kwa mkulima ikiwemo kutofikisha Miwa kiwandani kwa wakati au kutupwa kwa Miwa njiani kutokana na kuzidisha uzito wa miwa Kwenye gari.
Naye Bi. Elizabeth Masheyo kwa niaba ya wakulima na wanakijiji wa kijiji Cha Sanje ameshauri Makandarasi kuweka Kambi zao Kijijini hapo na kuajiri wavunaji wa Miwa wanaoishi katika eneo hilo ili kuwezesha shughuli zingine za kiuchumi kujua Kijijini hapo ikiwemo kuinua mzunguko wa pesa kwani kwa sasa mzunguko wa pesa umekuwa mdogo kwa kuwa wakataji miwa wengi hawatoki Kijijini hapo bali wanatoka eneo jirani la Ruaha.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.