Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela amepiga marufuku wafugaji mkoani humo kuingiza mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima na kuharibu mazao huku akiahdi kukomesha tabia ya wafugaji kulisha mashamba ya wakulima na kulipa faini kwani amesema tabia hiyo inaendeleza migogoro katika Mkoa huo.
Martine Shigela ametoa maelekezo hayo Juni 12 mwaka huu alipotembelea skimu ya umwagiliaji ya Itete iliyoko Wilayani Malinyi ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake Wilayani humo inayolenga kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi.
Shigela amesema baadhi ya wafugaji wamekuwa wakiamini kuwa wana fedha za kulipa faini, pale mifugo yao itakapokamatwa, kwa sababu hiyo hawachukui hatua za makusudi kuzuia mifugo yao kuingia kwenye mashamba ya wakulima wakitegemea kutoa fedha zao kwenye kesi hizo, kwa sababu hiyo Shigela ameelekeza kesi hizo zifikishwe mahakamani badala ya kulipa faini nje ya mahakama.
“Kwa hiyo nielekeze wale wafugaji watakaokuja kulisha na wakakiri kosa wakamlipa mkulima, mwenyekiti wa Kitongoji au mtaa, hizo pesa zipokeeni lakini andikeni barua mpelekeeni Mkuu wa Wilaya. hicho ndicho kitakuwa kielelezo cha kwamba huyo mfugaji aliingiza mifugo, tutampeleka mahakamani kama sehemu ya jinai ya kuhatarisha Amani kwenye eneo husika” ameagiza Shigela.
Wananchi wa Wilaya ya Malinyi hususan wa Skimu hiyo ya umwagiliaji mara nyingi wamekuwa wakilalamikia kero ya mifugo eneo ambalo Disemba 27, 2021 yalitokea mauaji ya mkulima mmoja yaliyosababishwa na migogoro ya pande hizo mbili za wakulima na wafugaji.
mwenyekiti wa jukwaa la mchele Wilaya ya Malinyi ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha wakulima Mtimbira Bw. Ekusi Gabriel Ngapulila pamoja na kumshukuru Rais Samia suluhu Hassani kwa kuunga mkono jitihada za wakulima kwa kuwapatia Skimu ya Itete ametaja changamoto katika kilimo hicho cha umwagiliaji kuwa ni mifugo kuharibu mazao yao husuan mpunga jambo ambalo linapelekea kukata tamaa ya kilimo hicho.
Mwenyekiti huyo kwa naiaba ya wakulima wenzake ameiomba serikali kuweka mkakati kabambe wa kuhakikisha mifugo haiingii kwenye mashamba yao au kuwatengea wafugaji maeneo yao na kuomba kuchukua hatua za makusudi na za haraka pale wanapotoa taarifa ya uvamizi wa wafugaji kurisha mashamba yao.
Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mathayo Massele amebainisha kuwa Skimu hiyo ina gharama ya shilingi 6.092 Bil. Kwa ajili ya kulima hekta 8,000 lakini hadi sasa zinazolimwa ni hekta 1,000 pekee.
Aidha, amebainisha kuwa sababu kubwa ya mifugo kuja katika skimu hiyo ni ukosefu wa maji kwa hao mifugo hivyo amesema wanaendelea kutafuta majawabu ya kudumu kwa ajili ya mifugo hao ili wasiweze kufika katika skimu hiyo.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa huyo ametembelea mradi wa kituo cha Afya cha Itete kilichopewa fedha kiasi cha shilingi 250 Mil. na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 93.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa amemuelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi Joanfaith Kataraia kuwaachia wananchi wanaokizunguka Kituo hicho cha Afya ardhi ekari 20 kati ya 35 zilizopo sasa na kuwalipa fidia wananchi wenye ekari 15 zinazotumika kujenga majengo yake ili kuondoa kero na migogoro baina yao na wananchi na Serikali inayoweza kujitokeza siku za baade kwa kuwa eneo la ekari 15 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha Afya kwa vijijini ni eneo toshelevu.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.