Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela ameupongeza Uongozi wa Kiwanda cha Sukari cha Kilombero kilichopo Mkoani humo kwa kukubali kutenga fedha zinazotokana na mapato ya kila mwaka ya kiwanda hicho kwa ajili ya kuimarisha huduma za jamii katika maeneo yanayozunguka Kiwanda hicho.
Shigela ametoa pongezi hizo mbele ya wananchi wa kata ya Ruaha Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Mkoani humo wakati wa Mkutano wa hadhara uliowakutanisha wananchi, Viongozi wa vijiji, Kata na Halmashauri Pamoja na Uongozi wa Kiwanda cha Sukari cha Kilombero uliofanyika Aprili 24 mwaka huu katika Uwanja wa Wazi wa kata hiyo.
Hatua hiyo ya Mkuu wa Mkoa ya kutoa pongezi hizo imekuja baada ya kutoa fursa kwa Wananchi zaidi ya 300 waliokusanyika katika Mkutano huo kueleza changamoto zinazowakabili katika kata yao ambapo wamebainisha kwamba Kata hiyo inakabiliwa na changamoto za miundombinu ya barabara, Afya, maji, Ukosefu wa Ofisi za kutolea huduma za jamii ikiwemo ofisi za Serikali za mitaa Pamoja na uchakavu wa gari la Polisi la Kituo cha Polisi cha Kata hiyo.
Kutokana na Changamoto hizo Mkurugenzi wa Idara ya mahusiano Kiwanda cha Sukari cha Kilombero Ephraim Mafuru amewaeleza wananchi wa Kata hiyo kwamba kiwanda hicho kitatenga fedha zaidi ya Millioni 400 kila mwaka kwa ajili ya kuimarisha huduma za jamii katika maeneo yote yanayozunguka Kiwanda hicho ikiwa sambamba na wale ambao wanapakana na mashamba ya miwa ya Kiwanda.
Aidha Mafuru amebainisha kwamba wananchi wa maeneo hayo wamekuwa na mchango mkubwa katika uendeshaji wa kiwanda cha Sukari cha Kilombero hivyo Fedha hizo zinastahili kuimarisha miundombinu katika maeneo yao kama sehemu ya kutambua mchango wao kwa kiwanda hicho.
Naye Meneja Masuala ya biashara wa Kiwanda hicho Bruno Daniel ameahidi kushughulikia taratibu zote za utoaji ajira kiwandani hapo ili wananchi wa maeneo hayo wapate kipaumbele cha kunufaika na ajira za kiwandani hapo kila zinapojitokeza. Amesema katika miradi mbalimbali inayobuniwa na kiwanda hicho ikiwemo mpango wa ujenzi wa kiwanda kipya cha Kilombero (K3) watahakikisha kwamba wananchi wa maeneo yote jirani na eneo la kiwanda ikiwa sambamba na wale wanaopakana na mashamba ya miwa wanapata nafasi katika ajira zinazozalishwa kiwandani hapo.
Ahadi hizo za Uongozi wa Kiwanda hicho ndizo zilizomuinua Mkuu wa Mkoa Martine Shigela na kuupongeza Uongozi wa Kiwanda na kusisitiza kwamba jambo hilo litaimarisha Uhusiano mwema uliopo kati ya Kiwanda na Wananchi wa maeneo ya vijiji na kata zilizopo upande wa Halmashauri ya Kilosa na Kilombero ambao wamepitiwa na maeneo ya Kiwanda hicho.
Katika hatua Nyingine, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela amewataka viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa wakiwemo viongozi wa mabaraza ya Ardhi ya Kata na Halmashauri kushughulikia haraka tatizo la migogoro ya Ardhi iliyopo kwenye Kata ya Ruaha na Kilosa kwa jumla ili wananchi wa maeneo hayo waendelee na shughuli zao za Kijamii.
Baada ya Mkutano huo, Shigela ameendelea na ziara yake katika Kata ya Sanje iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero ambayo ni miongoni mwa maeneo yanayopakana na mashamba ya miwa ya Kiwanda cha Sukari cha Kilombero na kuwaeleza wananchi wa kata hiyo kwamba changamoto zilizopo katika vyama vya Ushirika vya wakulima wa miwa zimeshatafutiwa ufumbuzi.
Amesema ujio wake katika Kata hiyo na nyingine zinazopakana na Kiwanda cha Sukari cha Kilombero ni maalum kwa kusikiliza na kuzitatua changamoto zilizojitokeza akitambua kwamba wananchi wa maeneo hayo ni wakulima wakubwa wa miwa inayotumiwa na Kiwanda hicho.
Hata hivyo amewasisitiza wakazi hao wa Sanje na wananchi wa Mkoa wa Morogoro kwa jumla kuendelea kutoa ushirikiano katika zoezi la uandikishaji wa Anwani za makazi linaloendelea Pamoja na kujiandaa na zoezi la Sensa ya watu na makazi linalotarajiwa kufanyika mwezi Agosti Mwaka huu.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.