SHIGELA ATOA MAELEKEZO MAZITO
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela amewataka viongozi wa Serikali na Taasisi zake Mkoani humo hususan wanaohusika na kupandisha madaraja ya watumishi kufanya hivyo bila kusukumwa na bila kusubiri muda wa mwishoni uliotolewa na Serikali wa kupandisha madaraja hayo kwa watumishi wanaostahili.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela (wa tatu kulia) akitoa zawadi na cheti kwa mmoja wa Mfanyakazi Bora Marijani Mwaya anayefanya kazi kutoka katika Ofisi yake
Shigela ametoa agizo hilo Mei Mosi mwaka huu wakati wa maadhimisho ya siku ya Wafanya kazi duniani ambayo huadhimishwa Mei Mosi kila mwaka ambapo Kwa Mkoa wa Morogoro sherehe hizo zimefanyika Mikumi Wilayani Kilosa.
“Ipo tabia ya kusubiri dakika za mwisho ndipo tunaanza kukumbushana muda wa promotion unanataka kuisha, kwa hiyo niombe sana Maafisa Utumishi mfanye hivyo, na kwa kweli naamanisha wala sitanii”. ameagiza Shigela.
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati za Ulinzi na Usalama walioshiriki maadhimisho ya Mei Mosi
Meza Kuu wakiwemo Wabunge Mhe. Profesa Paramagamba Kabudi Mbunge wa Jimbo la Kilosa (kulia) na Mhe. Denis Londo wa Jimbo la Mikumi (wa pili kulia). kushoto kabisa Ni Dkt. Rozalia Rwegasira Kaimu Katibu Tawala (RAS) Mkoa wa Morogoro. wengine ni viongozi wa shirikisho la vyama vya Wafanyakazi TUCTA
Mkuu huyo wa Mkoa amewataka Maafisa Utumishi kutekeleza majukumu yao ya kupandisha na kushusha vyeo vya watumishi bila kumuonea yeyote wala kuangalia upande mmoja wa kushusha vyeo vya watumishi kuliko kuwapandisha na kuangalia stahili zao.
Mbali na maagizo hayo Mkuu huyo wa Mkoa amekemea kwa baadhi ya Wakuu wa Taasisi, Idara na halmashauri ambao hawajibiki kupeleka zawadi za wafanya kazi bora siku yasherehe ya Mei Mosi ambao wamewachagua badala yake kuahidi kulipwa siku nyingine jambo ambalo ametaka lisirudiwe tena.
Wasanii wa Mashairi wenye ulemavu wa kuona wakiimba shairi lao lililokuwa na maudhui ya Mei Mosi ambalo liliwagusa watu wengi
RC Shigela akiwa katika picha ya pamoja na waimba mashairi
watu waliwatunza waimba mashairi
MKuu wa Mkoa akishirikiana na Kaimu RAS kuhesabu michango ya fedha iliyotolewa kwa ajili ya washairi
Sambamba na hayo Martine Shigela amewataka waajiri wa watumishi wa Umma kuwaruhusu wafanyakazi wao kuwa na vyama vyao mahali pa kazi lakini pia kuwaruhusu kushiriki sherehe za Mei Mosi.
Katika hatua nyingine Kiongozi huyo amewataka wafanyakazi nao kufanya kazi kwa bidii na kutekeleza majukumu waliyopewa kwa weledi na uaminifu masaa yote ya kazi ili kuiletea maendeleo Taasisi husika na Taifa zima kwa ujumla.
Burudani nyingine zilikuwepo. hapo ni umoja wa wasanii wa muziki kutoka Kilosa wakiburudisha na meza kuu kujikuta wako jukwaani
Shirikisho la vyama vya wafanyakazi Tanzania TUCTA kupitia Risara yao iliyosomwa na Katibu wa TALGWU Mkoa wa Morogoro Bi. Hellen Kobelo mbele ya mgeni rasmi imeeleza changamoto mbalimbali ambazo bado zinawakabili watumishi Serikalini na Sekta binafsi ikiwemo kero ya kutopandishwa vyeo au madaraja kwa wakati pamoja na kucheleweshewa kurekebishiwa mishara kwa wale waliopandishwa na kwamba upandishwaji huo wa madaraja umekuwa si wa weledi.
Aidha, wameiomba serikali kuiagiza Idara ya kazi na Uhamiaji kuendelea kufanya kaguzi za mara kwa mara kwenye sehemu za kazi hasa mashambani na migodini ili kubaini uhalali wa wageni wanaofanya kazi katika maeneo mbalimbali hapa nchini na kuchunguza mikataba na vibali walivyo navyo.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kilosa Profesa Paramagamba Kabudi mbali na kuwahakikishia watumishi kuwa yeye pamoja na wabunge wengine watahakikisha wanawapambana kwa ajili ya maslahi yao ya kiutumishi ambayo bado hawajatekelezewa amesema watumie fursa ya filamu ya Royal Tour iliyozinduliwa hivi karibu na Mhe. Samia Suluhu Hassan kutangaza Mbuga ya wanyama ya Mikumi.
Wahe. Wabunge wa Jimbo la Kilosa (kulia) na Jimbo la Mikumi Dennis Londo
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kilosa Yohana Kasitila (mwenye trucksuit) akipongezwa na Mkuu wake wa Wilaya hiyo Majid Mwanga kwa kutambuliwa kwake kuwa mmoja wa wafanya kazi Bora
Mwisho, amewahamasisha wawekezaji wazawa kuwekeza katika mji wa Mikumi na Kilosa kujenga hoteli zenye viwango vya juu kwa ajili ya watalii watakaoanza kumiminika katika Mbuga hiyo baada ya kuhamasishwa na filamu ya Royal Tour.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.