RC shigela awashauri Bodaboda Gairo, atoa mwezi mmoja kwa wenye pikipiki zenye usajiri feki
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela ametoa mwezi mmoja kwa waendesha pikipiki maarufu kama Bodaboda Wilayani Gairo kusajili pikipiki zao kihalali kwani imefahamika kuwa baadhi ya waendesha pikipiki hao pikipiki zao zina usajili ulioandikwa kwa mkono ambapo ni kinyume cha sheria.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela
Martine Shigela ametoa agizo hilo wakati wa Mkutano wa Hadhara na wananchi wa Mji wa Gairo ikiwa ni mara ya kwanza KWA Mkuu huyo kuongea nao wananchi hao tangu ateuliwe na Mhe. Samia Suluhu Hassani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuuongoza Mkoa wa Morogoro.
Katika hotuba yake Mkuu huyo wa Mkoa amesema, Wilaya ya Gairo ni moja ya Wilaya zenye changamoto ya uhalifu ukiwemo wizi wa pikipiki ambao mara kadhaa umepelekea baadhi yao kupoteza pikipiki zao na hata maisha yao kwa kukodiwa na baadhi ya wahalifu na kisha kuwapora pikipiki na kuuawa.
Mhe, Martine Shigela RC Morogoro akiteta jambo na Katibu Tawala wa Mkoa huo Mariam Mtunguja (kushoto)
Kwa sababu hiyo Shigela amewataka Bodaboda wote Wilayani Gairo kwanza, kuwa makini na watu wanaowabeba na kuwataka wawapeleke maeneo tofauti, lakini pili bodaboda hao wanapaswa kutoa ushirikiano kwa Serikali, kwa maana ya polisi na kutoa taarifa zenye uhakika katika kukabiliana na wahalifu hao ili wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Hata hivyo Martine Shigela ametoa mwezi mmoja kwa pikipiki zote ambazo hazijasajiliwa ama zimesajiliwa isivyo halali kusajili pikipiki hizo ndani ya kipindi cha mwezi mmoja kuanzia Juni 14 mwaka huu, vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa wataobainika wana pikipiki zisizo na usajili halali au zimesajiliwa isivyo halali.
“Nipongeze kamati ya Ulinzi na usalama ya Wilaya, nipongeze na DC umeshatoa maelekezo mahususi na maelekezo haya ni maelekezo ya Mkoa mzima wa Morogoro, kama kuna pikipiki zimeandikwa kwa mkono na wakati tunahangaika kuwatafuta wezi…..tunawapa ndani ya mwezi mmoja wazisajili kihalali” ameagiza Martine Shigela.
Akimkaribisha Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Gairo Siriel Mchembe yeye aliwahakikishia wananchi namna Serikali ya awamu ya sita ilivyojidhatiti katika kupunguza kero kwa wananchi na kutoa mfano wa hivi karibuni ambapo Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alivyopunguza faini za makosa ya bodaboda kutoke shilingi elfu thelathini hadi elfu kumi.
Mkuu wa Wilaya ya Gairo Siriel Mchembe
Kabla ya Mkuu wa Mkoa kupewa fursa ya kuongea, wananchi wa Gairo walitoa kero wanazokabiliana nazo ikiwa ni pamoja uwepo wa wizi wa pikipiki hususana katika kata ya Magoleko, pamoja na kamata kamata ya bodaboda inayofanywa na Polisi Wilayani humo jambo ambalo tayari Mhe. Mkuu wa Mkoa amepiga marufuku kuwakamata hovyo vijana hao tena wakiwa wamevaa kiraia.
RC Martine Shigela akivishwa skafu na vijana wa sakauti
RC na DC Gairo wakionekana wakicheza wakati wakikaribishwa uwanjani kwa ajili ya Mkutano
Changamoto nyingine ambazo wananchi waliziwasilisha mbele ya Mkuu wa Mkoa ni pamoja na upungufu wa dawa katika kituo cha Afya cha Gairo na kukosekana wa gari la kubebea wagonjwa (Ambulance) katika kituo hicho.
Rachel Nyangasa (kulia) Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo wakati wa mkutano wa hadhara
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.