RC SHIGELA AAGIZA TAASISZA ZA KISERIKALI KUJIFUNZA UWEZESHAJI KUPITIA MAONESHO YA TANO YANAYOENDELEA MOROGORO
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela ameziagiza Taasisi za Kiserikali Mkoani humo kushiriki na kujifunza mambo mbalimbali ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kupitia maonesho ya Mifuko ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi yanayoendelea Mkoani humo.
Martine Shigela ametoa agizo hilo leo Mei 9 mwaka huu kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro (RAS) wakati akifungua Maonesho hayo ya tano yanayofanyika katika viwanja vya Jamhuri katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesema ni lazima kwa Taasisi za Serikali kutenga muda na kwenda kujifunza katika Maonesho hayo ili kujua ni kwa namna gani Wananchi wanaowaongoza wananufaika na Mifuko hiyo ya Uwezeshaji Kiuchumi.
“Lakini kwa Mkoa Katibu Tawala uko hapa, Wataalamu wetu wanaohusika na hizi Sekta ambazo ziko hapa za Uwezeshaji iwe ni Uzalishaji ambako wewe mwenyewe ndio Inchaji wa Sekta zinazohusika na Uzalishaji iwe ni Viwanda, iwe ni Kilimo, Misitu, Maliasili, Uvuvi na Mifugo lazima tutenge muda wa kuja kujifunza ili tujue namna gani Wananchi wananufaika na hii Mifuko, tujue wapi imetekelezwa ndani ya Mkoa wetu”. Amesema Mkuu wa Mkoa Martine Shigela.
Katika hatua nyingine Martine Shigela ameiagiza Mifuko ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kuwasaidia Wakulima wadogo ili waweze kuinuka Kiuchumi kwa lengo la kuleta tija kwa mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla hasa katika kukuza pato la Taifa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albart Msando ametoa wito kwa Madiwani wote wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kuhudhuri maonesho hayo na kujifunza kuhusu Mifuko hiyo namna inavyofanya kazi na jinsi Wananchi wananufaika moja kwa moja na mifuko hiyo ya Uwezeshaji.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Bi. Beng’i Issa amebainisha kuwa hadi kufikia Mwezi Machi Mwaka huu Mifuko hiyo ya Uwezeshaji imefanikisha Mikopo na ruzuku ya zaidi Shilingi trilioni 5.38 kwa Wajasilismsli zaidi ya milioni 8 wakiwemo wanawake milioni 4.5.
Akiweka wazi changamoto zinazowapata wakulima wadogo Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Kuchochea Kilimo Tanzania Bw. John Kyaruzi amaesema changamoto kubwa kwa wakulima hao ni kukosa mitaji ya kutosha, riba kubwa katika mabenki na ukosefu wa masoko ya mazao yatokanayo na kilimo hapa nchini hivyo,mfuko wa TACTS uko tayari kutatua kero hizo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.