SHIGELA AAGIZA JESHI LA POLISI KUMKAMATA ANAYEDHULUM WANANCHI WA MLIMBA
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela ameliagiza jeshi la Polisi Mkoani humo kumkamata mara moja Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mkuyuni kata ya Chisano Tarafa ya Mlimba Wilayani Kilombero Bw. Kassim Mlawa kwa tuhuma ya matumizi mabaya ya madaraka na kudhulumu wananchi maeneo yao yakiwemo mashamba.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela akitatua changamoto za wananchi wa Mlimba Wilayani Kilombero ambapo alitoa agizo kwa Jeshi la Polisi kumkamata Bw. Kassim Mlawa kwa tuhuma za kudhulumu wananchi.
Martine shigela ametoa agizo hilo Julai 19 mwaka huu akiwa katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Tarafa ya Mlimba Wilayani Kilombero ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya siku tano ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi wa Wilaya ya Kilombero.
Siku ya pili ya ziara hii anakutana na wananchi wa Mlimba ambapo alishuhudia wananchi wengi wakimlalamikia Mwenyekiti wa kitongoji cha Mkuyuni Kassim Mlawa kunyang’anya mashamba ya watu kwa kutumia cheo chake cha uenyekiti wa Kitongoji.
Moja ya watu walioathiriwa na dhuluma za mwenyekiti huyo ni pamoja na Bibi Sarah Nyalusi wa kitongoji hicho cha Mkuyuni ambaye alimweleza Mkuu wa Mkoa kuwa alinyang’anywa mashamba yake pamoja na fedha taslimu shilingi 310,000/= jambo ambalo kiongozi huyo hakupendezwa nalo.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela akimpatia pesa za kujikimu Bi. Sarah Nyalusi wakati wa Mkutano na wananchi wa Mlimba.
Kwa sababu hiyo aliliagiza jeshi la polisi Mkoani humo kumkamata Bw. Kassim Mlawa na kubaki naye kituo kikuu cha Polisi cha Mkoa huo ili aweze kuhojiwa na kujibu tuhuma zinazoelekezwa kwake ikiwa ni pamoja na kugawa kiholela ardhi iyorudishwa kutoka TAWA.
“Sasa huyu mlawa wa Mkuyuni huko, kesho nimuone yuko mjini, na kamishna hilo eneo lililorudishwa na TAWA lirudishwe kwenye kijiji na wale wote waliopewa ardhi hiyo kinyemela na Mlawa tunawafuta wote na tutakuja kugawa kwa wananchi kwa usawa” aliagiza Martine shigela.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi ambaye ni Kamanda wa Jeshi hilo Mkoa wa Morogoro Fortunatus Musilim akihutubia wananchi wakati wa Mkutano huo.
Katika hatua nyingine Shigela alimuagiza Kamanda jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro SACP Fortunatus Muslim kuhakikisha mtuhumiwa huyo anarejesha fedha za Bibi Sarah shilingi 310,000 alizochukua huku akitumia fursa hiyo kuwaomba viongozi waliokuwa katika msafara wake kumchangia Bibi sarah mchango wa fedha na kufanikiwa kupata jumla ya shilingi 451,000 na kumkabidhi bibi huyo.
Kwa upande wa Mbunge wa Jimbo la Mlimba Mhe. Godwin Kunambi alisema Mwenyekiti huyo alionekana kama Mungu mtu katika eneo hilo la Mkuyuni na anatamani mtuhumiwa huyo achukuliwe hatua kali za Kisheria ikiwa ni pamoja na kufungwa jela akibainika na hatia.
Mhe. Mbunge wa jimbo la Mlimba Godwin Kunambi akimkabidhi pesa Bi. Sarah Nyalusi wakati wa ziara hiyo ya Mkuu wa Mkoa.
Naye Bibi Sarah Nyalusi alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kwa kutatua kero yake ya muda mrefu huku akifika mbali zaidi kwa kumuombea Mama Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuteua viongozi waadilifu na wenye kutoa msaada kwa wananchi.
Baadhi ya wananchi wa Tarafa ya Mlimba waliojitokeza wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Julai 19 mwaka huu.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.