SIMBACHAWENE AAGIZA SHUGHULI ZINAZOFANYIKA NANENANE KUWA ENDELEVU
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Uratibu na Bunge George Simbachawene ameagiza shughuli za maonesho zinazofanyika viwanja vya nanenane ziwe endelevu kwa mwaka mzima ili kufanya eneo hilo kuwa kitovu cha teknolojia katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.
Waziri Simbachawene ametoa agizo hilo leo Agosti 8 mwaka huu wakati akifunga maonesho ya Wakulima maarufu kama nanenane Kanda ya Mashariki yaliyofanyika katika viwanja vya mwalimu Julius Kambarage Nyerere vilivyopo Nanenane Katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Akizungumza kwa niaba ya Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla kwenye maonesho hayo ya nanenane kanda ya mashariki yanayoshirikisha mikoa ya Tanga, Pwani, Dar es Salaam na Morogoro, Waziri Simbachawene ametoa wito wa kusambaza kwa wananchi teknolojia mpya za kilimo, Mifugo na Uvuvi ili kukuza uchumi wao huku akitaka akitaka shughuli hizo kuwa endelevu kwa mwaka mzima
Katika hatua nyingine Waziri Simbachawene amewataka Viongozi wa ngazi mbalimbali wa Mikoa hiyo minne kutekeleza Maagizo ya viongozi wote waliotembelea maonesho ya mwaka huu waliyoyatoa wakati wakitembelea maonesho hayo.
Mwisho, Waziri George Simbachawene ameagiza maonesho hayo ya nanenane yatumike kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo katika Sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi ili kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Kilimo Anthon Mavunde ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzanaia Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza Bajeti ya Wizara ya Kilimo kutoka shilingi Bil. 294 kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022 hadi shilingi Bil. 954 kwa bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023.
Aidha, amesema Wizara hiyo ipo kwenye mipango ya kuendeleza kilimo cha umwagiliaji na tayari wameanza kuyapitia mabonde makubwa 22 hapa nchini yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji na kuyafanyia utafiti ili kujenga miradi mikubwa ya umwagiliaji
Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Mwassa amejikita akiongea katika hafla hiyo amesema Mkoa umejipanga kukomesha changamoto kubwa inayoukabili Mkoa wa Morogoro ambayo ni Migogoro ya Wakulima na Wafugaji na kwamba wanajipanga kutenganisha maeneo ya wakulima na wafugaji ili kukomesha migogoro hiyo.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Mkoa wa Morogoro Fatma Mwassa amesema maonesho ya Nanenane ya mwaka huu pamoja na kuwa yamechelewa kuanza amebainisha kuwa takribani wananchi 70,000 kutoka sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi wametembelea maonesho hayo.
Maonesho ya Nanenane ya mwaka huu yaliyokuwa na kaulimbiu ya ajenda ya kumi ya thelathini, Kilimo ni Biashara, shiriki kuhesabiwa kwa mipango Bora ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi yamehitimishwa rasmi leo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Uratibu na Bunge Mhe. George Simbachawene
MWISHO
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.