Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adama Kighoma Malima amemuagiza Meneja wa shamba la SUMA JKT Mngeta Plantation lililoko Wilayani Kilombero Mkoani humo Meja Gaudensi Msaka kuandaa Mpango mkakati utakaoonesha uendelezaji wa shamba hilo lenye ukubwa wa ekari 12,000 kwa lengo la kukuza sekta ya kilimo hapa nchini.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima ( wa pili kushoto) akiwa pamoja na Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa ( wa kwanza kulia), Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Mhe. Danstan Kyobya na Meja Gaudensi Msaka kwenye shamba la mpunga.
Mhe. Adam Malima ametoa agizo hilo Juni 8 mwaka huu akiwa Wilayani Kilombero wakati wa ziara ya kutembelea Halmashauri zote tisa za Mkoa huo na kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa kila Halmashauri hizo.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima akijaribu moja kati ya mitambo inayotumika katika shughuli za uzalishaji katika shamba hilo.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema, kuendeleza shamba hilo, inahitaji uwekezaji mkubwa kwa sababu hiyo amemtaka Meneja wa shamba hilo na viongozi husika wa shamba la JKT SUMA Mngeta Plantation kuandaa andiko litakaloonesha namna ya kuboresha uendeshaji wa shamba hilo kwa tija.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima akijionea shughuli mbalimbali za uzalishaji zinazofanywa na SUMA JKT.
“...nimeongea nao na nimewaambia wakatengeneze andiko la kuendeleza ekari 10,000 kati ya ekari 12,000 za shamba hili...” amesema Mhe. Adam Malima.
Aidha, Mhe. Adam Malima amesema benki za hapa nchini zina uwezo wa kutoa fedha ambazo zinaweza kutumika katika kuendeleza shamba hilo.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa ameonesha kufarijika kuona shamba hilo liaendelezwa na SUMA JKT na namna Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilivyojithatiti kuwatumikia wananchi wake.
Kwa upande wake Meneja wa shamba la SUMA JKT Mngeta Plantation Meja Gaudensi Msaka amesema kuwa mpango wao kwa sasa ni kuwashirikisha wataalam mbalimbali wa kilimo wa ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa mazao yanayolimwa kwenye shamba hilo kutoka gunia 15 hadi kufikia gunia 30 au zaidi.
Baadhi ya mitambo inayotumika katika shamba la Mngeta Plantation.
Amesema, kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2022/2023 uongozi ulipanga kulima ekari 5,500 ambapo tayari ekari 2,000 za mpunga zimeshalimwa, huku wakiwa katika maandalizi ya kulima ekari 3,500 za mahindi na msimu wa mwaka 2023/2024 wanatarajia kulima ekari 9,000 huku msimu wa 2024/2025 wanatarajia kulima ekari zote 12,000 ambapo ekari 7000 ni za mahindi na ekari 5,000 zitalimwa mpunga.
Awali shamba la SUMA JKT Mngeta Plantation lilikuwa likiendeshwa na KILOMBERO PLANTATION Ltd (KPL) na sasa linaendeshwa na SUMA JKT wakizalisha mazao ya mpunga na mahindi.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.