Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa – TAKUKURU Mkoani humo kufuatilia matumizi mabaya ya fedha za Serikali zaidi ya Shilingi Mil. 500,000,000/= zilizotumika katika ujenzi wa kituo cha Afya cha Duthumi kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro.
Agizo hilo amelitoa Machi 12, mwaka huu wakati wa ziara yake ya kikazi Wilayani humo ya kukagua miradi ya maendeleo ya sekta ya Afya na Elimu ambapo alifika katika kituo hicho cha Afya, kukagua maendeleo ya ujenzi wake na kugundua ubadhirifu wa fedha hizo.
Loata Sanare amesema kuwa Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa Shilingi Mil. 500,000,000/= kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya kituo hicho cha Afya ambapo fedha hiyo ilitumika bila kukamilisha majengo yaliyokusudiwa.
Aidha, amesema licha ya fedha iliyotolewa na Mhe. Dkt. John Pomnbe Magufuli kutokamilisha majengo hayo, Halmashauri iliongezea Shilingi Mil. 72,000,000/= zilizotokana na mapato ili kukamilisha ujenzi wa majengo hayo ambapo kwa mara nyingine Mkurugenzi akalazimika kuongeza silingi Mil. 25,000,000/=.
‘’Kila kituo cha Afya wametoa Milioni 400, na baadhi ya maeneo kwa sababu ya umbali walipewa Milion 500, na hapa kukawa na ubadhilifu mkubwa wa fedha hali iliyopelekea baadhi ya watu kuchukuliwa hatua, na Milion 100 mliyoongezea ingetosha kukamilisha majengo yote muhimu’’ amesema Loata Sanare
Wakati wa ziaya yake katika eneo hilo la Duthumi wananchi walipata fursa ya kutoa changamoto zinazowakabili ambapo kati yake hizo walimuomba Mkuu wa Mkoa gari la kubebea wagonjwa (Ambulance) kwa ajili ya ya kituo cha Afya Duthumi.
Wakielezea mateso wanayopata Bi. Mwanahawa Mohamed, amesema licha ya kituo hicho kuhudumia Tarafa mbili za Bwakila chini na Mvuha hakuna gari la wagonjwa hivyo wagonjwa wakizidiwa hulazimika kutafuta gari kutoka Mamlaka ya uhifadhi wa Wanyama Pori Tanzania - TAWA au kutoka tarafa ya Ngerengere ambayo iko mbali na Kituo hicho.
Changamoto nyingine iliyowasilishwa mbele ya Mkuu wa Mkoa na Chesco Raulent ni wauguzi kuchelewesha kutoa kibali maalumu (Rufaa) kwa wagonjwa waliozidiwa kwenda kupata huduma ngazi ya Hospitali ya Wilaya, hali ambayo hupelekea wagonjwa kupoteza maisha.
Kwa upande wake Kaimu DMO wa kituo hicho Kasole Maungo, amekiri kuwepo kwa changamoto ya gari ya wagonjwa ambapo amesema TAMISEMI inatarajia kutoa magari ya wagonjwa matano moja kati ya hayo italetwa katika kituo cha Afya Duthumi.
‘’Kuna vituo vitano ambavyo TAMISEMI wamesema yatakuja magari katika vituo vitano na kituo ambacho kitapewa gari mpya ni hiki hapa, kwahiyo kuhusu Ambulance TAMISEMI italeta’’ amesema Maungo .
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.