Kufuatia jitihada mbalimbali zinazofanywa na taasisi za kidini hapa nchini katika kuwahudumia wananchi, Serikali imezipongeza na kuzihamasisha taasisi hizo kuendelea na juhudi hizo za kuwaletea maendeleo wananchi wake.
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. Shaka Hamdu Shaka (kulia) akiwa pamoja na Shekhe Mkuu wa Jumuiya ya Waislamu wa Ahmadiyya nchini wakisikiliza salamu kutoka kwa viongozi wa dini kwenye hafla ya kuadhimisha miaka 134 ya kuzaliwa kwa Jumuiya ya Ahmadiyya.
Pongezi hizo zimetolewa Machi 19 mwaka huu na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. Shaka Hamdu Shaka kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwassa wakati akizungumza na viongozi wa dini pamoja na wananchi kwenye hafla ya kuadhimisha miaka 134 ya kuanzishwa kwa Jumuiya ya Waislamu wa Ahmadiyya hapa nchini iliyofanyika katika viwanja vya msikiti wa Ahmadiyya uliopo katika Manispaa ya Morogoro.
Mhe. Shaka amesema Serikali inatambua mchango na jitihada za taasisi za dini katika kufanikisha maendeleo ndani ya Mkoa huo na taifa kwa ujumla. Akitolea mfano Jumuiya ya waislamu wa Ahmadiyya Mkoani Morogoro amesema Jumuiya hiyo imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya nchi kwenye sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, na maji kwa kuchimba visima katika maeneo mbalimbali ndani ya Mkoa huo.
"...lakini Serikali inathamini namna ambavyo mnavyounganisha nguvu katika kuleta maendeleo na mfano mzuri ni kwa Jumuiya ya Ahmadiyya pamoja na madhehebu mengine..." amesema Mhe. Shaka Hamdu Shaka.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya amewahakikishia viongozi wa dini Mkoani humo kuwa Serikali itaendelea kuheshimu na kuthamini michango inayotolewa na taasisi hizo za kidini Ili kuongeza kasi ya kuwaletea wananchi Maendeleo.
Nae Shekhe Mkuu wa Jumuiya ya Waislamu Wa Ahmadiyya nchini Tanzania Bw. Tahir Mahmood Chaudhry ameishukuru na kuipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuruhusu uhuru wa kuabudu, hivyo ni nchi ya kusifiwa na kujivunia kwenye hili kwa sababu zipo nchi duniani hazina uhuru wa kuabudu.
Kwa upande wake Shekhe Saidi Hamadi Kondo mwakilishi wa Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Shekhe Twaha Kilango amewataka viongozi wa dini, Serikali na Wazazi kushirikiana ili kupambana na vitendo vya ukatili kwa watoto, hivyo elimu itolewe kwenye nyumba za Ibada na mashuleni ili kuwakinga watoto hao dhidi ya vitendo hivyo.
Jumuiya hiyo ya Waislamu wa Ahmadiyya ilianzishwa mwaka 1886 na Leo imetimiza miaka 134 tangu kuanzishwa kwake, hafla ya maadhimisho hayo imehudhuriwa na wajumbe wa kamati ya Haki na Amani ya Mkoa, kamati ya Maridhiano ya Mkoa na Jumuiya ya Waislamu wa Bohora Mkoani humo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.