Taasisi za kibenki zatakiwa kutafuta mbinu mpya za kuwasaidia wakulima.
Taasisi za kibenki hapa nchini zimetakiwa kutafuta mbinu na utaratibu mzuri utakaosaidia wakulima kupata mikopo yao kwa wakati na kwa masharti nafuu ili kuendeleza kilimo chenye tija na kukuza uchumi wao na uchumi wa nchi kwa ujumla.
Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde (Mbunge) Januari 28 mwaka huu wakati wa kikao kazi cha viongozi wa vyama vya ushirika vya wakulima wa Miwa hapa nchini (Agricultural Marketing Cooperative Society - AMCOS) na Taasisi za kibenki kilichofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Sukari cha Taifa kilichopo Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro.
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Anthony Mavunde akiwa kwenye kikao kazi baina ya wakulima wa miwa na taasisi za kibenki, Mkoani Morogoro, Januari 28 mwaka huu
Agizo hilo limekuja baada ya viongozi wa vyama hivyo kumweleza Naibu Waziri changamoto wanazokutana nazo mara wanapohitaji mikopo kwenye taasisi za kibenki ikiwa ni pamoja na riba kubwa, masharti mengi pamoja na kupata mikopo hiyo wakati msimu wa kilimo umeshapita.
Kwa sababu hiyo, Naibu Waziri Mavunde amezitaka Taasisi hizo za kibenki, kila benki kwa namna yake kutafuta utaratibu unafaa kwao na unaoweza kushawishi wakulima kwenda kukopa lakini mikopo itakayotoka wakati wa kilimo au muda walioomba wakopaji na si vinginevyo.
“ kwenu ninyi mabenki ndio wakati mwafaka sasa, mmeshaona changamoto kubwa inayosemwa ni namna ya kuweza kutoa mikopo kwa wakati ili wakulima wawahi msimu. njooni na utaratibu ambao utamfanya mkulima awe confortable kuja kwako. Lakini mwongozo wetu ni kwamba lazima mikopo yetu iendane na msimu wa mazao ya wakulima ili wasipishane nao” amesisitiza Naibu Waziri Mavunde.
Mhe. Mavunde akipokelewa na baadhi ya viongozi mkoani Morogoro wakati wa ziara yake, kulia ni Mrajisi msaidizi Mkoa wa Morogoro Kenneth Shemdoe
Aidha, pamoja na Serikali kupongezwa kutokana na kuazishamfumo mpya wa uvunaji miwa Kijiografia (ZONE), Naibu Waziri ameiagiza Bodi ya Sukari hapa nchini kwa kushirikiana na Vyama vya Ushirika kuanzisha mfumo huo mpya wa uvunaji miwa kijiografia katika maeneo mengine yenye wakulima wadogo wa miwa lengo likiwa ni kukomesha changamoto mbalimbali zilizokuwa zinajitokeza hapo awali.
Wakiwa katika kikao hicho, baadhi ya Viongozi wamelalamikia suala la Ukomo wa Madeni ambapo Naibu Waziri Mhe. Anthony Mavunde amemwelekeza Mrajisi wa Vyama vya Ushirika hapa nchini kushughulikia suala hilo haraka ili mkulima asinyimwe fursa ya kukopesheka katIka taasisi za kibenki kwa sababu ya changamoto ya ukomo wa madeni.
Baadhi ya Viongozi wa vyama vya ushirika (AMCOS) vya wakulima wa zao la miwa wakiwa kwenye kikao kazi kilichofanyika Chuo cha sukari cha Taifa Mkoani Morogoro
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mikumi Mhe. Denis Londo amemueleza Naibu Waziri changamoto ya wakulima wa miwa kuwa ni pamoja na pembejeo za kilimo kuwa juu hususan Mbolea lakini pia mbolea hizo kutopatikana kwa wakati na kumuomba Waziri kuichukua changamoto hiyo na kwenda kuifanyia kazi.
Mbunge wa jimbo la Mikumi Mhe. Denis Londo
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari hapa nchini Prof. Kenneth Bengesi kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri, aliwaeleza wajumbe nia ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, kuendelea na mpango wa kupanua viwanda vya Sukari vya Kilombero, Mtibwa na Kagera ili kuondoa changamoto ya upatikanji wa sukari hapa nchini.
Mkurugenzi wa bodi ya sukari Tanzania Prof. Kenneth Bengesi akiongea wakati wa kikao hicho
Awali, Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia Uchumi na uzalishaji Mali Mkoa wa Morogoro Dkt. Rozalia Rwegasira amemshukuru Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Anthony Mavunde kwa kufanya ziara katika mkoa huo na kutoa maaelekezo ya serikali ambapo alikiri kuwa watayatekeleza yote na kwa wakati.
Aidha, Dkt. Rozalia amesema zao la miwa mkoani humo linategemewa zaidi na kufafanua kuwa takribani tani 1,700,000 zinazalishwa kwa mwaka na zao linalofuata ni mpunga linalozalisha tani 900,000 kwa mwaka na kumjulisha Waziri kuwa mkoa huo una chakula cha ziada tani 1,300,000.
Dkt. Rozalia Rwegasira akiongea katika kikao hicho
Kwa upande wa wakulima wa miwa akiwemo Habibu Nakanoga ambaye ni Katibu wa Miwa AMCOS Kilombero wameipongeza serikali kwa kuanzisha utaratibu wa uvunaji miwa kwa kuzingatia jiografia (ZONE) na kusema kuwa utaratibu huo umeonekana una tija kubwa kwa wakulima wa miwa wa Kilombero ambapo msimu huu wameonekana kufanya vizuri ukilinganisha na misimu iliyopita.
Mkulima wa miwa Leonard Deogratias kutoka Misenyi Mkoani Kagera ambaye ni mwenyekiti wa AMCOS ya Bubale, pamoja na kuzitaka Taasisi za kibenki kuwafikia na kuwakopesha kama wanavyofanya kwa wakulima wa miwa wa Morogoro pia ameomba uongozi wa Bodi ya Sukari na Serikali kwa jumla kwenda kuwatengenezea utaratibu wa ZONE ili kuondosha changamoto walizo nazo.
Baadhi ya Viongozi wa vyama vya wakulima wa miwa wakiwa katika picha ya pamoja na Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Anthony Mavunde (Katikati ya waliokaa)
Kwa mujibu wa Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Bw. Kenneth Shemdoe ametaja baadhi ya faida za uvunaji miwa kwa kutumia utaratibu wa Kijiografia (Zonning) kuwa ni pamoja na kusaidia kudhibiti magonjwa kwenye mazao ya miwa, kwa kuwa kazi hiyo hufanywa kwa pamoja kama zone badala ya mtu mmoja mmoja.
Mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika Kenneth Shemdoe kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro akimsikiliza kwa makini Naibu Waziri wa Kilimo (Hayupo pichani) wakati wa kikao cha wadau wa kilimo cha zao la miwa
Faida nyingine alizozitaja za mfumo wa uvunaji miwa kijiografia ni pamoja na urahisi wa kupitisha miundombinu, kupunguza changamoto za mioto, wepesi wa kupata takwimu sahihi za uzalishaji wa zao la miwa pamoja na kukomesha tabia ya utoaji na upokeaji rushwa wakati wa mavuno ya zao hilo.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.