Hivi karibuni Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa maelekezo kwa Taasisi zote hapa nchini zinazohudumia chakula watu zaidi ya 100 kusitisha matumizi ya kuni za kupikia chakula, badala yake alielekeza taasisi hizo kuanza kutumia Nishati Safi ya Kupikia, lengo likiwa ni kupunguza uharibifu wa mazingira unaotokana na ukataji miti kwa ajili ya kupata kuni na hivyo kusababisha mabadiliko ya tabia nchi.
Kutokana na agizo hilo la Serikali, Kampuni ya Taifa Gas imeamua kuunga mkono agizo hilo la Serikali kwa asilimia mia moja na kuanza mara moja utekelezaji kwa kutembelea Taasisi mbalimbali hapa nchini ili kuhamasisha na kujitangaza ili taasisi hizo ziweze kutumia bidhaa yao ya Taifa Gas.
Leo hii Taifa Gas wapo hapa Mkoani Morogoro katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ambapo wametembelea Taasisi mbalimbali kuona kama taasisi hizo zimeanza kutekeleza agizo la Serikali na kama wanahitaji huduma yao.
Mengi zaidi ungana na Meneja Mauzo wa Taifa Gas Bw. Moses Masawe ambaye anaeleza kwa kina lengo la wao kuwepo hapa Morogoro lakini pia anabainisha athari zitokanazo na matumizi ya kuni na mwisho anatoa wito kwa jamii katika kutekeleza agizo la Serikali na namna walivyojipanga kuwahudumia wananchi katika kuwapatia Nishati ya Gesi Safi.
Baadhi ya taasisi zilizotembelewa katika zoezi hilo ni Pamoja na Morogoro Hoteli, Morogoro Sekondari, Shule ya Msingi Mlimani na shule ya Msingi Bungo. Taasisi nyingine ni shule ya Msingi Mchikichini A na Mchikichini B, pamona Chuo cha Mamlaka ya Elimu na Mafunzo stadi - VETA cha hapa Mkoani Morogoro
Pamoja na changamoto chache zilizojitokeza, kimsingi Taasisi zote zilizotembelewa leo wanakubaliana na uamuzi huo wa Serikali na wako tayari kutekeleza agizo hilo.
MWISHO
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.