Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amezipongeza Wakala ya Barabara Tanzania - TANROADS na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini - TARURA Mkoani humo kwa jitihada za kurejesha miundombinu ya barabara pamoja na madaraja ambayo yaliharibiwa na mvua zilizonyesha kuanzia mwezi Disemba 2023.
Mhe. Malima ametoa pongezi hizo Machi 12, 2024 wakati akifungua kikao cha 41 cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Morogoro ambacho kimefanyika katika ukumbi wa Magadu uliopo halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema Mvua kubwa zilizonyesha kuanzia mwezi Disemba Mkoani humo zilisababisha uharibifu wa mali na miundombinu mbalimbali ikiwemo barabara na madaraja huku akibainisha kuwa TANROADS na TARURA kwa kushirikiana na taasisi nyingine zilifanya jitihada za kurejesha miundombinu hiyo kwa wakati.
"...nichukue nafasi hii kuwapongeza wataalam wetu wa TANROADS na TARURA na wengine ambao mlishiriki kupambana na kurejesha miundombinu ya barabara, ninawashukuru sana..." amesema Mkuu wa Mkoa.
Aidha, Mhe. Malima amebainisha kuwa Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa fedha nyingi kwenye utekelezaji wa miradi ya barabara kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2021/2022 akitolea mfano bajeti ya TANROADS kwa mwaka wa fedha 2022/2023 bajeti ya matengenezo ya barabara ilikuwa shilingi Bil. 24 na kwa mwaka 2023/2024 ni shilingi Bi. 20.7.
Kwa upande wa TARURA amesema kwa mwaka wa fedha 2022/2023 taasisi hiyo iliidhinishiwa kiasi cha shilingi Bil.26.96 kwa ajili ya matengenezo na miradi ya maendeleo ya barabara na kwa 2023/2024 ilitengewa shilingi Bil. 26.58.
Sambamba na hilo Mhe. Malima ametoa wito kwa wananchi Mkoani humo kulinda na kuhifadhi miundombinu ya barabara na kuwataka viongozi katika maeneo yao kuwachukulia hatua wale wote watakaobainika kujihusisha na uharibifu wa miundombinu ya barabara.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amewata Wakuu wa Wilaya, Wenyeviti wa Halmashauri na Wakurugenzi kwenda kusikiliza kero za wafanyabiashara waliopo katika maeneo yao.
Naye, Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Morogoro Mhandisi Geofrey Mtakubwa amesema kwa mwaka wa fedha 2023/2024 TANROADS imeidhinishiwa kiasi cha shilingi Bil. 24.292 kwa ajili ya matengenezo ya barabara na madaraja na miradi ya maendeleo Mkoani humo ambapo miradi mikubwa ya Kitaifa ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami inatarajiwa kutekelezwa.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Mhe. Pascal Kihanga ameutaka uongozi wa TARURA kuangalia namna ya kuzifanyia maboresho barabara za mitaa mbalimbali katika Manispaa hiyo ambapo amebainisha kuwa nyingi hazipitiki kwa usafiri wa gari huku akisema kuwa ubovu wa barabara hizo unasababisha wananchi kushindwa kufika maeneo yenye huduma muhim hivyo kukosa imani na Serikali yao.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.