Tanzania yasaini mkataba na china mradi wa soya.
Tanzania imeingia makubaliano ya kuanzisha mradi wa kilimo cha zao la Soya na Jamhuri ya watu wa China utakaotekelezwa hapa nchini na kisha China kununua zao hilo lengo likiwa ni kuongeza kipato cha wakulima na kuboresha hali ya lishe kwa wananchi wa maeneo ambayo mradi utatekelezwa na taifa kwa jumla.
Mkuu wa Wilaya ya Ulanga Ngollo Malenya (kushoto) akifungua washa ya tathmini ya mradi wa kilimo cha mahindi kwa tija na kutambulisha rasmi mradi wa kilimo cha zao la soya
picha ya pamoja ya washiriki wa washa hiyo
Hayo yabainishwa Novemba 16 mwaka huu na Mkurugenzi Msadidizi uingizaji wa mazao, masuala ya pembejeo na Ushirika kutoka Wizara ya Kilimo Bw. Beatus Malema wakati wa warsha ya tathmini ya mradi wa kuongeza tija kwenye zao la mahindi ambao umefikia kikomo chake, warsha ambayo pia imelenga kutambulisha rasmi Mradi mpya wa kilimo cha zao la maharagwe aina ya Soya.
Mkurugenzi Msadidizi wa uingizaji wa mazao, masuala ya pembejeo na Ushirika kutoka Wizara ya Kilimo Bw. Beatus Malema
Warsha hiyo iliendeshwa kwa njia ya video conference moja kwa moja kutoka china, hapa ni baadhi ya viongozi wa china wakiwa kwenye washa hiyo wakiwa china
Akiwa katika warsha hiyo ya siku moja iliyofanyika Mkoani hapa Bw. Malema amesema baada ya mradi wa mahindi kuisha muda wake unaofuata sasa ni mradi wa Soya ambapo Tanzania tayari imesaini mikataba ya kuiuzia China soya kupitia makampuni 81 ambayo tayari yamebainishwa kuiuzia nchi hiyo zao hilo la SOYA, hivyo amesema ni furasa kwa watanzania hususan wana Morogoro ambao tayari wana ushirikiano wa siku nyingi na China katika masuala ya kilimo kuitumia fursa hiyo Adhimu.
Maafisa Ugani na baadhi ya wakulima walioshiriki warsha hiyo.
Akibainisha zaidi Bw. Malema amesema Tanzania siku za nyuma ilikuwa inazalisha zao hilo kwa wingi ambapo pia walilenga kufikisha kuzalishaji wa tani milioni mbili kwa msimu kama fursa zote zingetumika vizuri, hata hivyo changamoto kubwa amesema ilikuwa ni upatikanaji wa soko ambapo kwa sasa soko limepatikana nchini china hivyo ni fursa kwa nchi kupeleka zao hilo huko.
Aidha, Bw. Malema amebainisha umuhimu wa zao hilo la soyo kuwa lina linatumika kwa kiwango kikubwa kwenye ufugaji wa kuku, samaki na mifugo minginekilimo hicho kinategemea sana zao hili kwa kuwa lina virutubishi vya kutosha (wingi wa Protini) ukichanganya na mahindi ambayo watu wamelalamika kuwa hayana soko unapelekea wawekezaji mkubwa kwa wanaotengeneza vyakula vya mifugo ambapo ametumia fursa hiyo kuwakaribisha kuwekeza hapa nchini.
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Hanji Godigodi (katikati) na Mkuu wa Wilaya ya Gairo Jabil Makame kulia wakifuatilia hotuba ya viongozi kutoka China kupitia simu ya kiganjani. kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mathayo Massele
Mwisho, Malema ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa makampuni yaliyosajiliwa kuuza soya nchini China nao kuingia mkataba na wakulima wa Tanzania ili kuongeza upatikanaji wa uhakika wa zao hilo kwa ajili ya kusafirisha China huku akibainisha kuwa wametoa wigo mpana kwa makampuni mbalimbali kutoka nchi za nje kuingiza mbegu za zao hilo ili kuleta mafanikio ya mradi huo kwa manufaa ya nchi hizo mbili.
“hapa naomba niongeze kitu kingine baada ya kuingia mkataba na haya makampuni tunayataka sasa yaweze kuingia kilimo cha mkataba na wakulima wetu ili kuweza kupata ‘volume’ ya kutosha ya soya na kuweza kusafirisha nchini China…”
Akifungua warsha hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Ulanga Ngollo Malenya kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Martine Shigela, amesema mradi huo mpya wa zao la Soya unaotarajiwa kuanzishwa ni mwendelezo wa ushirikiano wa nchi ya China na Tanzania kupitia Mkoa wa Morogoro katika mradi wa kuongeza tija kwenye zao la mahindi ambao umefikia kikomo chake mwaka huu.
Sambamba na hayo, Ngollo Malenye ametumia fursa hiyo kumjulisha Balozi wa China hapa nchini Bi. Wang Ke, kuwa Mkoa wa Morogoro ni Mkoa wenye fursa nyingi za uwekezaji katika Kilimo na Nyanja mbalimbali za kiuchumi, hivyo amekaribisha wawekezaji kutoka nchini mwake kuja kuwekeza hapa nchini hususan katika Mkoa wa Morogoro.
Aidha, Mhe. Ngollo Malenya amesema kuanzishwa kwa mradi huo wa kilimo cha zao la soya utaimarisha upatikanaji wa Lishe bora pamoja na kuwaongezea kipato wakulima wadogo ambao watashiriki katika mradi huo hivyo ametumia fursa hiyo kuishukuru nchi ya China kwa ushirikiano na msaada huo.
“Mradi huo utajikita katika uzalishaji na kuongeza thamani ya zao hilo ili kuwasaidia wananchi kuimarisha lishe, kuongeza kipato katika kaya za wakulima wadogo, angalau wakulima mia moja watafundishwa kilimo bora cha soya, kuongeza thamani ya soya kwa kuzalisha maziwa ya soya, unga wa soya na majani ya soya.”amesema Mkuu huyo wa Wilaya.
Sambamba na hilo Mhe,mgeni rasmi aliwaagiza wananchi kushiriki kikamirifu ili mradi huo uweze kukua na kuongezeka katika halmashauri nyiingine za mkoa huo.
“Naomba nitumie nafasi hii kuagiza kushiriki kikamirifu katika utekelezaji wa mradi huu na kuweka mikakati ya kuhakikisha kuwa mradi unakuwa endelevu na kuongezeka kwa wakulima wengine katika halmashauri za mkoa wetu.”
Kwa upande wake mratibu wa mradi wa kilimo cha mahindi kwa tija katika vijiji 10 vilivyokuwa vinatekeleza mradi huo Mkoani Morogoro kwa ushirikiano wa Tanzania na China Bw. Ernest Mkongo, amesema mradi wa zao la soya unatarajia kuanza mwanzoni mwa msimu huu wa mvua.
Amesema mradi huo utaongeza thamani ya zao la soya na matarajio ya mradi ni kuanza na wakulima 100, lengo likiwa ni kuongeza kipato kwa wakulima hao na kuboresha hali ya lishe kwa washiriki, mradi huo utaanza kwanza kutekelezwa kwa vijiji vinne vya Makuyu (Mvomero), Mtego wa simba (Morogoro DC), Peapea na Kitete (Kilosa).
Mratibu wa Mradi wa Kilimo cha Mahindi kwa tija Bw, Ernest Mkongo
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro ambaye pia ni Katibu Tawala msaidizi Uchumi na Uzalishaji Mali Dr. Rozalia Rwegasira akimkaribisha Mgeni rasmi kufungua warsha hiyo
Aidha, amebainisha kuwa mradi huo kwa kuanzia utagharimu dolla za Marekani elfu 54 na baadae mradi utaendelezwa kadri mafanikio yatavyokuwa yanapatikana huku akibainisha kuwa kila kijiji tajwa hapo juu, kitakuwa na wakulima 25 ambao watapewa mafunzo, mbegu na baadae mashine za kutengeneza bidhaa za zao hilo la soya.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mlimba Mhandisi Stephen Kaliwa (mbele) akifuatilia kwa makini warsha hiyo
Nao wakulima waliopata mafanikio kupitia mradi wa kilimo cha mahindi kwa tija walioshiriki washa hiyo akiwemo Bi. Luja Lugomola wamekiri kuwa mradi umewazesha kuongeza kipato chao na kusaidia kujenga nyumba kwa ajili ya makazi pamoja na kuwasomesha watoto wao shule hadi vyuo vikuu baada ya kufanikiwa kuvuna mahindi gunia 18 kwa hekari moja kutoka gunia 4 kwa hekari walizokuwa wanavuna kabla ya mradi huo ambao umetumia uzoefu na utalaamu wa kulima mahindi kutoka nchini China
Mkoa wa morogoro kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Sokoinne cha Kilimo (SUA) kwa upande wa Tanzania na Chuo Kikuu cha Kilimo cha China kwa upande wa China ulianzisha Mahusiano ya kimaendeleo tangu mwaka 2011 kwa kutekeleza mradi wa kilimo cha mahindi kwa tija kutoka vijiji viwili vya Peapea Wilayani Kilosa na Mtego wa Simba Wilaya ya Morogoro na baadae mradi ulikua hadi kufikia vijiji nane vilivyopatikana karibu kila Wilaya za Mkoa huo.
Baadhi ya Maafisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa walishiriki washa hiyo
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.