Timu ya soka ya RAS Morogoro yaididimiza Viwanda.
Ikiwa ni siku ya pili tangu michezo ya SHIMIWI kuanza kutimua vumbi Mkoani Morogoro, timu ya soka ‘RAS Morogoro’ imeonesha kiwango bora cha mchezo wake na kuibuka kidedea kwa kuibugiza timu ya Wizara ya Viwanda na Biashara mabao 3 – 1 mchezo uliochezwa katika uwanja wa Jamhuri wa Mjini Morogoro.
Mashindano hayo ya SHIMIWI ambayo yanaonekana kuanza kupata msisimko zaidi yameendelea leo huku miamba watatu wakipimana ubavu ikiwemo timu ya RAS Morogoro.
Katika mchezo wa kwanza timu ya RAS Morogoro imeididimiza timu ya Wizara ya Viwanda na Biashara mabao hayo na kupelekea timu hiyo kunyakua alama zote tatu huku ikijiwekea mazingira mazuri kwenye msiamamo wa kundi lake, kundi A lenye timu tano ambazo ni Maliasili, Mahakama, Viwanda, Kilimo na wenyeji RAS Morogoro.
Mabao hayo yote matatu (Hat – trick) ya timu ya RAS Morogoro yamewekwa kimiani na Said Chijana ambaye ni kiungo mshambuliaji ambapo bao la kwanza lilipatikana kwa njia ya penati katika kipindi cha kwanza na mabao mawili yakifungwa kwa ustadi mkubwa.
Kesho Oktoba 22 wenyeji hao wanatarajia kucheza mchezo wao wa pili dhidi ya timu ya Mahakama, nayo timu ya Kilimo itachuana na timu ya Maliasili.
Mechi nyingine zilizochezwa leo Oktoba 21 ni TAMISEMI dhidi ya RAS Dar es Salaam ambapo TAMISEMI imeibuka na ushindi wa magoli mawili kwa sufuri, huku timu ya RAS Mara ikiisambaratisha timu ya NFRA kwa matokeo ambayo hadi mwandishi wa habari hizi anaondoka uwanjani hapo tayari NFRA ilikuwa imepokea kichapo cha magoli saba kwa nunge.
Kipa huyu balaa, unene wake usikutishe
Licha ya mashindano hayo ya SHIMIWI kuendelea kufana Mkoani humo, zoezi la utoaji chanjo ya UVIKO – 19 nalo liliendelea kufanyika ndani ya Uwanja wa Jamhuri kwa ajili ya kuendeleza mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Viongozi wa Kamati ya michezo ya SHIMIWI kutoka RAS Morogoro Mwl. Musa Mnyeti na Grace Njau wakiteta jambo mara baada ya mechi
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.