Mamlaka ya dawa na vifaa tiba Tanzania (TMDA) imekasimisha mamlaka ya ukaguzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi kwa wataalamu wa maabara, Wafamasia na waganga wa mifugo wa Halmashauri kwa lengo la kukagua na kudhibiti changamoto ya bidhaa hizo kutumika pasipo na ubora.
Meneja wa TMDA Kanda ya Kati Bi. Sonia Mkumbwa akizungumza wakati wa mafunzo ya siku mbili ya wakaguzi wa dawa vifaa tiba, na vitendanishi wa Halmashauri za Mkoa wa Morogoro.
Hayo yamebainishwa na Meneja wa TMDA Kanda ya Kati Bi. Sonia Mkumbwa wakati wa mafunzo ya siku mbili ya wakaguzi wa dawa, Vifaa tiba na Vitendanishi wa Halmashauri za Mkoa wa Morogoro yaliyofanyika Ukumbi wa Bwalo la Umwema katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Bi. Sonia amesema lengo la kukasimu mamlaka hayo, pamoja na kuongeza Ushirikiano baina ya pande hizo mbili ni kuwajengea uwezo Wakaguzi hao katika kudhibiti Ubora wa Dawa na Vifaa tiba ili kulinda Afya za Watumiaji kwa kuwa wao wako Kitaifa na Kikanda na kwamba peke yao hawawezi kufika kila mahali kufanya shuguli hizo za ukaguzi wa dawa.
“kwa sababu TMDA iko Kitaifa na katika Ofisi za Kanda hatuwezi kufika katika kila Halmashauri na kuwa na Watumishi wetu” alibainisha Sonia Mkumbwa
Aidha, amesema lengo kubwa ni kuwasogezea wananchi huduma hiyo ukilinganisha ukubwa wa maeneo ya nchi hii na uchache wa watumisjhi wa TMDA hapa nchini ambao hawazidi 270 na hivyo ili kuongeza ufanisi zaidi wamefikia hatua ya kukasim Mamlaka yao kwa watumishi wa Halmashauri.
Afisa Mifugo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro Dkt. Gasper Msimbe akiwa katika mafunzo ya siku mbili ya wakaguzi wa dawa,vifaa tiba na vitendanishi wa Halmashauri za Mkoa wa Morogoro yaliyofunguliwa Juni 6 Mwaka huu.
Hata hivyo, Sonia amesema wakiwa katika kikao hicho, washiriki watapewa miongozo mbalimbali inayohusu utunzaji na usambazaji sahihi wa bidhaa hizo za Afya zikiwemo dawa, Vifaa Tiba na Vitendanishi namna ya kuziharibu mara baada ya kupoteza ubora unaohitajika kwa Binadamu.
Akifungua Mafunzo hayo Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Dkt. Rozaria Rwegasira pamoja na kushukuru TMDA kutao mafunzo kwa watalaamu hao amewataka TMDA awaendelee kuwajenge uwezo zaidi watalaam hao kwa kuwa Elimu haina mwisho na kwamba kadri watakavyojengewa uwezo ndivyo watakuwa na uwezo wa kudhibiti madhara makubwa kwa binadamu yatokanayo na kutumia dawa zisizo na ubora.
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Rozalia Rwegasira akizungumza na wakaguzi wa TMDA katika mkutano na wakaguzi wa dawa, Vifaa tiba na Vitendanishi wa Halmashauri za Mkoa wa Morogoro, mkutano uliofanyika Juni 6 mwaka huu katika ukumbi wa Bwalo la Jkt Umwema.
Aidha Dkt. Rozaria amewataka washiriki ambao ndio wataalamu wa maabara, Wafamasia na waganga wa mifugo kufanya kazi kwa uaminifu na weledi zaidi ili kufikia malengo ya TMDA ya kukasimisha mamlaka yao Kwao kwa kulinda Afya za wananchi kwa kutoa huduma iliyo Bora na Salama.
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Rozalia Rwegasira (wa kwanza kushoto) akiwa na Afisa Mifugo wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Gasper Msimbe pamoja na Meneja wa TMDA Kanda ya Kati Dkt. Sonia Mkumbwa.
Nao washiriki wa Mafunzo hayo akiwemo Felisia Mapunda ambaye ni Mfamasia wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga pamoja na kuishukuru Serikali kupitia TMDA kushiriki mafunzo hayo amebainisha kuwa mafunzo hayo yatawasaidia kwenda kufanya kazi kwa weledi lakini zaidi kwenda kumlinda mwananchi kutopata dawa ambazo hazina ubora.
Picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo yaliyoandaliwa na TMDA yaliyofanyika ukumbi wa JKT Bwalo la Umwema Juni 6 mwaka huu Mkoani Morogoro.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.