Mamlaka ya Mapato nchini Tanzania (TRA) Mkoani Morogoro imezindua Wiki ya Huduma kwa mlipakodi ikiwa na lengo la kuboresha huduma zake kwa kuwakutanisha walipakodi na wataalam wa TRA ili kutatua changamoto zinazowakabili wakati wa ulipaji wa kodi.
Akizindua hafla hiyo Oktoba 03 mwaka huu iliyofanyika katika Ofisi za Mamlaka hiyo, Meneja wa TRA Mkoani humo Bw. Sylver Rutagwelera amesema lengo ni kumuwezesha mlipakodi kulipa kodi kwa urahisi kutokana na umuhim wa walipakodi hao.
Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoani Morogoro Bw. Sylver Rutagwelera (kushoto) akimlisha keki Makamu Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara Mkoani humo Prof. Faustin Lekule wakati wa hafla ya uzinduzi wiki ya Huduma kwa Mlipakodi Mkoani Morogoro.
“...leo tunazindua Wiki ya Huduma kwa Mlipakodi...Focus ya Mamlaka ni mlipakodi, namna gani tunamuwezesha huyu mtu kulipa kodi kiurahisi...” amesema Bw. Rutagwelera.
Aidha, Bw. Rutagwelera amebainisha kuwa TRA imelenga kuwafikia wateja wake kwa kusogeza huduma katika Wilaya za Mkoa huo, kuweka mifumo ya kisasa ambayo itawawezesha walipa kodi kulipa kodi zao katika maeneo waliyopo bila kufika ofisini.
Meneja huyo ameongeza kuwa Mamlaka ya Mapato Mkoani humo inapokea malalamiko, ushauri na changamoto za walipakodi wakati wote hivyo amewataka kufika katika Ofisi za TRA ili waweze kusikilizwa na kuhudumiwa.
Kwa upande wake Afisa Mfawidhi anayeshughulikia ushuru wa Forodha Bw. Shadrack Mbonea amewataka wafanyabiashara kuacha tabia ya kupitisha bidhaa kwa magendo bila kulipia ushuru na kukaguliwa ili kuepuka athari zitokanazo na bidhaa kama vile pombe kali na vipodozi. Pia, amesema kwa kufanya hivyo wanapunguza mapato ambayo Serikali ingeyatumia kuwaletea maendeleo wananchi wake.
Meneja wa TRA Mkoa wa Morogoro Bw. Sylver Rutagwelera akifurahia kinywaji pamoja na wadau mbalimbali wakati wa hafla ya uzinduzi wa Wiki ya Huduma kwa Mlipakodi.
Naye, Makamu Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoani Morogoro Prof. Faustin Lekule ameipongeza TRA Mkoani humo kwa kutoa elimu ya kodi kwa wafanyabiashara kwa kuwa elimu hiyo imesaidia kukuza mitaji yao ambapo kwa sasa wanapata mikopo kutoka taasisi mbalimbali za kifedha.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya walipa kodi Mkoani humo akiwemo Mkurugenzi wa Moro Batiki Dkt. Herriet Mkaanga amewataka wafanyabishara kulipa kodi ili Serikali iweze kutekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo hapa nchini.
Naye Bw. Dastan Mziwanda Mjasiliamali mdogo katika Manispaa ya Morogoro ameipongeza TRA kwa huduma bora huku akiwataka wataalam wa Mamlaka hiyo kuwafikia wafanyabiasha waliopo maeneo ya vijijini ili kuwapa elimu ya kodi.
Hawa ni baadhi ya wafanyakazi wa TRA Mkoani Morogoro wakiwa kwenye hafla ya uzinduzi wa Wiki ya Huduma kwa Mlipakodi.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.