Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amepongeza juhudi za Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Shirika la Reli Tanzania kuanzisha huduma za safari kwa kutumia Reli ya Mwendo kasi (SGR) kutoka Dar es salaam hadi Morogoro.
Mhe. Malima ametoa pongezi hizo Juni 14, 2024 baada ya kuwasili kwa treni hiyo katika stesheni ya reli iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Mkoani humo ikiwa ni mara yake ya kwanza kuanza rasmi kusafirisha abiria.
“… natumia fursa hii kuipongeza serikali lakini pia nalipongeza sana Shirika la Reli Tanzania kwa jambo kubwa walilolifanya…” amesema Mhe. Malima.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesema wananchi wanapaswa kutambua fursa zinazotokana na treni hiyo ili kuendana na kasi ya maendeleo inayotarajiwa na serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani mapinduzi ya teknolojia hapa nchini yanaendelea kurahisisha usafiri ili kuendesha shughuli mbalimbali kwa urahisi zikiwemo Kilimo, Biashara, na utalii.
Sambamba na hilo, Mhe. Adam Malima amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua umuhimu wa usafiri huo na kuhakikisha Juni 14 kuanza kufanya kazi ambapo kutaokoa upotevu mkubwa wa muda Pamoja na mapato ya serikalini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Bw. Masanja Kungu Kadogosa amesema kuwa katika utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha huduma za usafiri wa Treni zinakamilika na huduma za uendeshaji zinafanyika na kwamba loti ya kwanza Dar es Salaam - Morogoro na loti ya pili ya Dar es Sallm – Dodoma zote zinatakiwa kuwa zimekamilika ifikapo Julai 25, Mwaka huu.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mkuu amesema kuwa kuanza safari za treni za abiria kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro ni baada ya Shirika la Reli Tanzania kujiridhisha na utayari wa Miundombinu, Vitendea kazi (vichwa na Mabehewa) na mifumo ya Ishara na Mawasiliano.
Sambamba na hilo, Mkurugenzi Kadogosa amewataka wananchi kutumia huduma za usafiri wa treni kwani kupitia usafiri huo abiria wataweza kupata huduma zote ndani ya treni ikiwemo chakula, maliwato, mazingira mazuri ya kufanya kazi wakiwa safarini, huduma za mtandao pamoja na burudani.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la reli Tanzania Bw. Ally Karavina amesema kuwa kwa mara ya kwanza treni hiyo imeanza kusafirisha abiria na kuona wananchi wengi wamejitokeza kutumia usafiri huo huku akiwaasa kubadilika ili kuendana na usasa wa miundombinu hiyo hata kwa kuzingatia muda kwani treni hiyo huzingatia muda wa safari.
Bw. Karavina amewatoa hofu abiria kuwa shirika hilo lina vifaa vya kutosha kutosheleza abiria wengi zaidi hata ikibidi kununua treni nyingine ili kukidhi mahitaji ya wananchi.
Kwa niaba ya abiria Bw. Mbarouk Seif amefurahishwa na treni ya mwendokasi ya SGR kwa kuwa na huduma bora pamoja na kuzingatia muda kwani imetoka saa kumi na mbili kamili (12:00) na kufika saa moja na dakika Hamsini (1:50) na kumpongeza Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya kwa wananchi wake.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.