Tume ya kuangalia namna ya kubororesha Taasisi za Haki Jinai hapa nchini ambayo iliundwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kukusanya maoni juu ya kuboresha taasisi hizo imefanya kongamano lake Mkoani Morogoro na kukutana na wadau mbalimbali ili kupata maoni yao juu ya mapendekezo yaliyotolewa na tume hiyo kwa Mhe. Rais.
Hawa ni Wajumbe wa Tume ya kuboresha Taasisi za Haki Jinai wa kwanza kulia ni Mkuu wa Jeshi la Polisi Mstaafu IGP Ernest Mangu, Bw. Omary Issa, Mkuu wa Jeshi la Polisi Mstaafu IGP Said Mwema wakati wa Kongamano la haki jinai.
Tume hiyo imefanya Kongamano hilo Oktoba 27, 2023 lililolenga kukusanya maoni juu ya mapendekezo ya kuboresha taasisi za haki jinai hapa nchini, kongamano ambalo limefanyika katika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Mount Uluguru uliopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Akibainisha mapendekezo yaliyotolewa na Tume hiyo, Mkuu wa Jeshi la Polisi Mstaafu hapa nchini IGP Ernest Mangu amesema miongoni mwa mapendekezo waliyoyatoa ni pamoja na kuandaliwa mkakati wa kitaifa wa kubaini na kuzuia uhalifu, matumizi ya Tehama kwa taaisi zinazohusika na mifumo ya haki jinai, ukamataji wa waharifu kuachiwa jeshi la polisi, uwepo wa matumizi mabaya ya madaraka kwa baadhi ya watendaji wa Serikali na kuundwa kwa chombo cha kitaifa cha upelelezi.
Naye, Bw. Omary Issa ambaye ni Mjumbe wa Kamati hiyo amesema tume hiyo imekasimiwa madaraka na kuwa Kamati ya kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa mapendekezo kwa taasisi zenye mifumo ya haki jinai ambapo zinakadiliwa kufikia taasisi 18. Aidha, ameongeza kuwa baadhi ya mapendekezo hayo yatachukua muda mrefu katika utekelezaji wake na mengine yameshaanza kufanyiwa kazi.
Hawa ni baadhi ya wajumbe wa Tume ya kuboresha Taasisi za Haki Jinai kulia ni Bw. Omary Issa na mwengine ni Mkuu wa Jeshi la Polisi Mstaafu IGP Said Mwema wakiwa kwenye Kongamano la haki jinai.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima, ameishukuru Tume hiyo kwa umahili wao wa kufanya kazi, huku akimpongeza Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwateua watu wajumbe makini na kwamba kwa uthubutu na utendaji wao anaamini nia aliyoikusudia itatimia.
Nao baadhi ya Washiriki wa Kongamano hilo akiwemo Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Manispaa ya Morogoro Ndg. Fikiri Juma amependekeza kubadilisha jina la Magereza na kuitwa chuo cha mafunzo ili wafungwa wapate mafunzo badala ya mateso. Aidha, amependekeza kuwa Taasisi za kijeshi ziajiri Wataalam wa lugha ya alama ili kuwasaidia watanzania wenye matatizo ya kusikia kuweza kuwasiliana na wenzao kwa urahisi.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Manispaa ya Morogoro Ndg. Fikiri Juma akitoa maoni wakati wa Kongamano la haki jinai.
Tume ya kuboresha haki jinai iliundwa kwa lengo la kuangalia mfumo wa haki jinai na taasisi zake ili kubaini mapungufu yake na kisha kuja na mapendekezo ya kuuboresha.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.