Serikali Mkoani Morogoro ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Adam Kighoma Malima imedhamiria na inaendelea kuweka mikakati na mipango madhubuti kuhakikisha Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro inakuwa miongoni mwa Miji mikubwa hapa Nchni.
Hayo yamebainishwa Julai 2, 2024 na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Adam Kighoma Malima wakati wa kikao Maalum cha Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo cha kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kilichofanyika mkoani humo.
Mhe. Malima amesema kupitia ujio wa reli ya kisasa ya mwendo kasi (SGR) inakuwa chachu ya maendeleo katika Mkoa huo na itachangia kwa vikubwa Mkoa wa Morogoro kuwa jiji kwa sababu ya uwepo wa wasafiri wengi wanaopita mkoani humo ambao wataongeza mzunguko wa fedha na Halmashauri kujipatia mapato ya kutosha.
"...sasa nyie mkitaka kujiita city village ni nyie lakini mimi nataka Morogoro iitwe city council.." amesisitiza Mhe. Adam Malima.
Hata hivyo Mkuu huyo wa Mkoa amesema, Halmashauri hiyo haiwezi kuwa jiji kama ukusanyaji wa mapato ya ndani ni hafifu, pamoja na kuipongeza kuwa ndiyo Halmashauri inayoongoza kwa ukusanyaji wa mapato ya ndani kati ya Halmashauri zote za Mkoa huo, bado ameitaka Halmashauri hiyo kuweka mikakati ya kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa dhamira ya kukidhi moja ya vigezo vya kuwa jiji lakini pia kuwaletea wananchi maendeleo.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa amesema anasikitika sana kuona Halmashauri ya manispaa ya Morogoro inakuwa na mazingira machafu muda wote, likiwemo soka la Mawenzi. hivyo, amewataka watendaji kufanya jitihada na kutafuta mbinu mbadala za kutatua changamoto hiyo ya kuusafisha mji huo ili kuhakikisha mazingira ya manispaa hiyo yanakuwa safi.
Sanjari na hilo Dkt. Mussa amewataka watendaji wa Halmashauri hiyo kuhakikisha wanakusanya kodi kwa wafanyabiashara wote wa mji huo, kwani kuna kila dalili za manispaa hiyo kutokusanya kodi kwa baadhi ya wafanyabiashara au kama kodi hiyo inakusanywa basi haiingizwi kwenye mifuko ya Serikali.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Rebeca Nsemwa amesema Halmashauri hiyo ina mpango wa kuupanga mji huo kuwa wa kisasa zaidi ikiwa ni pamoja na kuondoa vibanda ambavyo vimekaa maeneo yasiyo sahihi, kupanga biashara mahali panapo stahili na kutoza faini kwa wale watakaobainika kuchafua mazingira ya manispaa hiyo ili kuhakikisha usafi unazingatiwa hususan kipindi hiki cha kujipanga kuelekea Morogoro kuitwa Jiji.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.