Kwa mara nyingine tena Bondia Twaha Ramadhan maarufu kama Twaha kiduku amekabidhiwa Bendera ya taifa kwa ajili ya kuuwakilisha Mkoa na Taifa kwa ujumla kushiriki pambano la masumbwi linalotarajiwa kufanyika Disemba 26 mwaka huu.
Twaha amekabidhiwa Bendera hiyo leo Disemba 24 Katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro na Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Mipango na Uratibu Ndugu Anza – Amen Ndossa kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa huo Mhandisi Emmanuel Kalobelo.
Pambano hilo la kipekee litahusisha Mabondia mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi ambapo Twaha Kiduku anatarajia kuzichapa na Bondia kutoka Jamhuri ya Demokrasia ya Congo Guy Tshimange katika uwanja wa Next door Arena Masaki mchezo wa roundi kumi uzito wa Kilo 76.
Akimkabidhi bendera hiyo Ndossa amesema, michezo hujenga Afya, hutumika kama kiungo cha upatanishi, michezo ni buruduni na kwa wakati wa sasa michezo ni Uchumi.
”Michezo hujenga afya, mchezo unatumika kama kiunga katika upatanishi, lakini kwa zama za sasa hivi mchezo ni sehemu ya kujipatia kipato yeye mwenyewe anayecheza, walimu wake, lakini na wale wote ambao wanahususika” amesisitiza Katibu Tawala huyo.
Kwa upande wake Kocha wa Bondia Kiduku Chanzi Mbwana, amesema jopo lake la ushindi limemuandaa vizuri Kiduku kumtwanga mpinzani wake hivyo wanamorogoro na watanzania wote watafurahia pambano hilo ambalo anaamini Twaha atapata ushindi mkubwa.
“Maandalizi ya Bondia wetu yapo vizuri, tumejiandaa kisaikoloji, teknically, kila kitu nikiwa na jopo langu la ushindi. Maana yake timu ushindi haijawahi kuangusha watu wa Morogoro.. anayeweza kuibeba bendera ya chuma ni Twaha peke yake hakuna mtu yoyote anaweza kuipeperusha bendera ya chuma” amesema Ndg. Chanzi
Naye Bondia Twaha Kiduku, amewatoa hofu Watanzania na kuwahakikishia kurudi na ubingwa licha ya watu wengi kuwa na wasiwasi juu ya msiba wa baba yake uliotokea hivi karibuni wakiamini pengine anaweza kushindwa kufanya vizuri.
Disemba 26 kila mwaka huadhimishwa siku ya mabondia duniani ambapo Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoshiriki.
MWISHO
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.