Maelfu ya Wananchi Mkoani Morogoro wamejitokeza kumpokea Mwanamasumbwi Twaha Ramadhani Kiduku wakati akirejea kutoka Jijini Dar es Salaam baada ya kuibuka Mshindi kwenye pambano lililofanyika Oktoba 30 Mwaka huu dhidi ya Bondia mwenzake kutoka Thailand.
Mapokezi hayo yamefanyika Novemba mosi Mwaka huu ambapo mapokezi hayo yalianzia Nanene katika Maispaa ya Morogoro kuelekea nyumbani kwake huku Umati wa watu ukifurika kumuunga Mkono na kumpongeza kwa ushindi huo.
Kiduku aliibuka Mshindi katika raundi ya saba baada ya kumchakaza bondia Sirimongkhon Lamthuam katika pambano la raundi 10 uzito wa Super Welter lililofanyika ukumbi wa PTA Saba Saba, barabara ya Kilwa, Jijini Dar es Salaam na kujinyakulia ubingwa wa Kimataifa wa WPC hivyo kuvunja rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kuchukua ubingwa huo.
Akizungumza na Waandishi wa habari mara baada ya kuwasiri Mkoani Morogoro, Kiduku amesema hajaridhika na ushindi huo hivyo ataendelea kupambana ili kuwa bingwa ndani na Nje ya Nchi huku akiutangaza Mkoa wa Morogoro na Tanzania kwa ujumla.
“Mimi nawaambia tu …..Bendera chuma Mlingoti chuma, bado sijaridhika na mapambano haya nahitaji kufanya vizuri zaidi ndani na nje ya Nchi show show” alisema Kiduku.
Aidha, bondia huyo ametoa shukrani kwa Wananchi wote wa Mkoa wa Morogoro waliojitokeza kumpokea na wadau mbalimbali waliomuunga Mkoano wakiwemo Babu Tale, Mbaraka Ali Said, Rashid Bodaboda na wengine ambao kwa namna moja au nyingine wamechangia kuibuka mshindi wa pambano hilo.
Kwa upande wake Kocha Charles Mbwana ametoa pongezi kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare na viongozi waandamizi wake kwa kuwakaribisha vizuri, kuwatendea haki Mabondia na kuwatuma kuleta Ubingwa katika Mkoa huo.
Naye Kaimu Afisa Michezo Mkoa wa Morogoro ambaye pia ni Afisa Vijana Mkoa wa Morogoro Bi. Winnifrida Madeba, ametoa shukrani kwa wadau waliojitokeza kumuunga mkono mwanamasumbwi huyo kuanzia maandalizi yake, wakati wa pambano hadi ubigwa unapatikana pamoja na mapokezi yake hapa Mkoani.
Pamoja na shukrani hizo Bi. Winnifrida ametoa ombi kwa wadau wa Michezo na wengine katika Mkoa wa Morogoro kujitokeza kushiriki katika Michezo mbalimbali na kuwasaidia Vijana kwani wao peke yao hawawezi kuleta mafanikio, hivyo serikali itaendelea kuunga mkono jitihada zao katika kuboresha Michezo Mkoani hapa ili vijana waweze kufikia ndoto zao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya Wananchi waliohudhuria kumpokea Mwanamasumbwi huyo akiwemo Shaabani Mahamud, amesema Kiduku amefanya maajabu ambayo hayajawahi kufanyika Mkoani hapa na ameutangaza vizuri Mkoa huu huku akitaka pambano kati ya Twaha na Mwakinyo.
Hii ni mara ya Pili kwa Mwanamasumbwi Twaha Kiduku kurejea na ubingwa Mkoani Morogoro ambapo mara ya kwanza alishinda shindano la kitaifa na sasa ameshinda shindano la Kimataifa.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.