Na Andrew Chimesela, Morogoro.
Mwanamasumbwi wa kimataifa Twaha Kiduku ametaja siri ya ushindi na mafanikio yake kuwa ni Morali aliyopewa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata ole Sanare huku akidai kuwa msingi mkubwa wa mafanikio hayo ni uwepo wa amani hapa nchini chini ya uongozi wa Dkt. John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Twaha Kiduku amesema hayo Novemba 3 Mwaka huu alipokwenda Ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kutoa shukrani zake kwa ushirikianao waliompa kabla na baada ya pambano lake la kimataifa la Oktoba 30 kati yake na Sirimongkhon Lamthuam kutoka Thailand ambalo lililomuwezesha kupata ushindi wa Technical Knock Out (TKO).
Akizungumza na waandishi wa habari Ofisini hapo Twaha kiduku ametoa shukrani kwa Loata Ole Sanare Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Katibu Tawala wa Mkoa huo Emmanuel Kalobelo na viongozi wengine kwa kumuunga mkono kabla na baada ya pambano lake.
“Ushindi huu umetokana na nguvu nyingi sana za Mkuu wangu wa Mkoa kunipa moyo na Viongozi wote wa Mkoa wa Morogoro, kwasababu najua pindi nilipokuwa naenda kuingia ulingoni Mkuu wa Mkoa wangu ananiangalia, RAS wangu wa morogoro ananiangalia na viongozi wote, pia Tanzania nzima inaniangalia hivyo nikasema siwezi kuuangusha Mkoa wangu na watanzania kwa ujumla” Alisema Kiduku.
Hata hivyo, Twaha Kiduku aliweka bayana kwa watanzania kuwa siri ya ushindi huo pia ni AMANI iliyopo hapa nchini ndiyo inayopelekea kila mtu anaendelea na shughuli zake na amani hiyo inatokana na uongozi madhubuti wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli wa Tanzania.
”Pia namshukuru sana Rais wetu John Pombe Magufuli kwa kuweka viongozi kuwa salama kwasababu laiti kama uongozi wake usingelikuwa imara sidhani kama pambano letu lingefanyika vizuri” Alisema Kiduku
Aidha, Kiduku amesema Desemba 26 Mwaka huu anatarajia kushiriki pambano la usiku wa Mabingwa wa kimataifa ambalo linahusisha Watanzania na mabondia kutoka Nje ya Nchi litakalofanyika Jijini Dar Es Salaam.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare amesema Mkoa wa Morogoro umepanga kuandaa miundombinu inayojitosheleza itayowezesha kila mwenye kipaji cha Mchezo wowote kushiriki na kusaidiwa katika kukuza kupaji hicho.
Sambamba na hilo, ametoa pongezi kwa Mwanamasumbwi huyo kwa kutimiza ahadi yake ya kurejea na ubingwa wa Kimataifa katika Mkoa wake kama ambavyo alikuwa amemuahidi Oktoba 27 Mwaka huu kabla ya kuelekea Jijini Dar es salaam kwa ajili ya pambano hilo.
Naye, Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Michezo Mkoani humo Mhandisi Emmanuel Kalobelo ametoa agizo kwa Halmashauri zote Mkoani humo kuandaa miundombinu kwa ajili ya Michezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Boxing.
Mhandisi huyo amesema Mkoa wa Morogoro umejipanga vizuri kuipa kiupaumbele Michezo huku akiwasihi vijana wenye vipaji katika mchezo wowote kujitokeza ili kutambua vipaji vyao na kuweza kuwasaidia wanamichezo wengine ambao hawafahamiki.
Pia, Mhandisi huyo ametoa ombi kwa Uongozi wa Twaha Kiduku kuunda Taasisi itakayo ongoza na kuratibu kazi anazozifanya mwanamasumbwi huyo ili kutunza rekodi ya matukio yote anayoyafanya na kutambulika kwa rasilimali watu ambao wanamuunga Mkono katika kazi zake.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.