Mwanamasumbwi maarufu wa ngumi za kulipwa Mkoani Morogoro Twaha Ramadhani almaarufu kama Twaha Kiduku ameagwa leo rasmi na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kuelekea kwenye pambano lake la ngumi baina yake na Dulla Mbabe linalotarajiwa kufanyika Agosti 20 mwaka huu Jijini Dar es Salaam.
Waliomuaga katika hafla hiyo fupi leo Agosti, 18 mwaka huu ni pamoja na mashabiki wa Twaha Kiduku, Menejimenti ya Kiduku pamoja na maafisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo wakiongozwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Bi. Mariam Mtunguja akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa huo Martine Shigela.
Akitoa nasaha kwa Mwanamasumbwi huyo, Bi. Mariam Mtunguja ambaye pia ni Mwenyekiti wa Michezo Mkoani humo, amemtaka Mwanamasumbwi Twaha Kiduku kutumia nafasi aliyonayo kutangaza vivutio mbalimbali vilivyopo katika Mkoa wa morogoro ili kuwavutia watalii wengi kuja nchini.
Amesema Mkoa wa Morogoro una vivutio vingi ambavyo watalii kutoka nje na ndani ya nchi wangelipenda kuviona zikiwemo mbuga za wanyama, mradi wa bwawa la Mwalimu Nyerere, mradi wa SGR na milima ya udzungwa.
‘’… Lakini Morogoro kuna fursa chungu nzima za uzalishaji, kwa hiyo wewe usiangalie ngumi tu, wewe utakachokizungumza wanakiamini, nikuombe sana utusaidie kuubeba Mkoa wa Morogoro kwa kututangazia vivutio vya utalii na fursa zilizopo katika Mkoa wa Morogoro…’’ ….amesema Bi. Mariam.
Kwa upande wake Twaha kiduku amemhakikishia Katibu Tawala huyo, Mkuu wa Mkoa Martine Shigela pamoja na mashabiki wote wa ngumi Mkoa wa Morogoro na Mikoa mingine kupata ushindi katika pambano hilo na kurudi na ushindi.
Amesema ushindi huo utatokana na hamasa ya pamoja aliyopewa na viongozi mbalimbali wa ndani ya Mkoa huo ikiwemo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kupitia Mratibu wake Afisa Michezo Bi. Grace Njau.
Naye, Afisa Michezo Mkoa wa Morogoro Bi. Grace Njau amewahakikishia wanamasumbwi wanaochipukia Mkoani humo kujitokeza kwenye mchezo huo kwani tayari Mkoa unaendelea kuwawekea mazingira mazuri ya kufanyia mazoezi ya ngumi ikiwa ni pamoja na eneo la DDC.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.