KAMATI ZA ULINZI NA USALAMA NA CMT, ZATAKIWA KUJADILI UKATILI, MIMBA NA NDOA ZA UTOTONI.
Kamati za Ulinzi na Usalama ngazi ya Wilaya na timu ya Menejeimenti za Halmashauri– CMT, zimetakiwa kuwa na utamaduni wa kujadili masuala ya Ukatili kwa watoto, mimba na ndoa za utotoni ili kuongeza kasi ya kupunguza au kumaliza kabisa matukio hayo ya kikatili yanayoendelea kuongezeka ndani ya jamii.
Wito huo umetolewa na Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Morogoro Bi.Jesca Kagunila wakati wa kufunga kikao kazi cha siku moja kilichofanyika Juni Mosi mwaka huu katika ukumbi wa mikutano wa Savoy Mjini Morogoro ikiwa ni mwendelezo wa vikao kazi vinavyofanyika kila baada ya miezi mitatu.
Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Morogoro, Jesca Kagunila, akisisitiza jambo wajumbe wa kikao, Juni Mosi, 2021
Bi Kagunila amesema Ukatili kwa watoto, mimba za utotoni na ndoa za utatoni ni ajenda inayotakiwa ijadiliwe na kila mtu badala ya kuwaachia Maafisa Ustawi wa Jamii pekee kwa kuwa Maafisa wa kada hiyo ni wachache ukilinganisha na matukio hayo yanayojitokeza kila kukicha hivyo nguvu ya pamoja inahitajika.
“Mimi natoa wito kwa Wakuu wa Wilaya pamoja na Wakurugenzi, kuwahimiza Maafisa Ustawi wa Jamii hasa kuwapatia takwimu zikiweza kujadiliwa katika vikao vya CMT, vikao vya Kamati za Ulinzi na Usalama itaweza kusaidia sana wao kuweka mikakati na kuelekeza nini kifanyike katika Halmashauri husika katika kulipunguza hilo tatizo au kuliondoa kabiasa hasa masuala ya mimba za utotoni na ndoa za utotoni pamoja na masuala ya ukatili..” amesema Bi. Jesca.
Katika hatua nyingine Bi .Jesca ametoa wito kwa halmashauri zote za Mkoa wa Morogoro kujenga au kutenga chumba kwa ajili ya kutolea huduma kwa wahanga wa ukatili, ndoa za utotoni na mimba za utotoni yaani “One stop Centre” ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wahanga kwa kuwa huduma hizo zitatolewa katika eneo moja lenye maafisa wote wanaohusika katika kumuhudumia.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dk. Kusirye Ukio ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi katika kikao hicho amewataka Maafisa Ustawi wa Jamii Mkoani humo kufanya kazi kwa juhudi na maarifa huku wakijijengea tabia ya kutathmini kazi zao kwa mujibu wa maelekezo ya Viongozi sambamba na kutumia kwa muda unaotakiwa fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kutekeleza majukumu yaliyo chini ya kada hiyo.
Mganga Mkuu wa Mkoa Dk. Kusirye Ukio akifungua kikao kazi cha Maafisa Usatawi wa Jamii
Naye Meneja wa Mradi wa Kizazi kipya Kanda ya Kati Bi. Merina Shaidi amebainisha lengo la mradi huo ni kutoa huduma kwa watoto waliothiriwa na walioathirika na Virus Vya Ukimwi – VVU, kutoa huduma za Afya, Elimu, lishe, uchumi, ulinzi na usalama kwa mtoto.
Meneja wa Mradi Bi. Merina Shaidi (kulia) akisikiliza kwa makini mada wakati wa kikao hicho
Pia, Bi. Merina amewataka Maafisa ustawi wa Jamii wakati wanapoelekea mwisho wa mradia huo kuendeleza kazi ambazo zimekuwa zikitekelezwa na mradi huo ili kuhakikisha taarifa za ustawi zilizopo kwenye kata zinahifadhiwa kwa usiri mkubwa ili ziweze kutumika wakati zitakapohitajika kama mwongozo wa Serikali unavyoelekeza.
Nao wajumbe wa kikao hicho akiwemo Bi. Ndayahundwa Bilama ambaye ni Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Morogoro amezitaka Halmashauri zote za Mkoa wa Morogoro kuangalia namna nzuri ya kubaini watu wenye ulemavu ndani ya Jamii ili kuunda vikundi vitakavyowawezeshwa kupata mikopo tofauti na sasa ambapo inaelezwa kuwa kundi hilo halipatikani ili kupatiwa mikopo jambo ambalo amelitilia shaka kama lina ukweli ndani yake.
Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba Neema Minanago amebainisha sababu ya kutotekelezwa kwa baadhi ya maazimio ya kikao kilichopita likiwemo suala la kujenga kituo cha kuhudumia waathirika wa Ukatili “One stop centre” katika Halmashauri, kuwa maelekezo ya awali hayakueleweka vema lakini kwa sasa wako tayari kwenda kutekeleza agizo hilo kwa kuwa limeelezwa vizuri na Mganga Mkuu wa Mkoa Dk. Kusirye Ukio.
Freedom Crispin, ambaye ni Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Halmashauri ya Mji wa Ifakara anakiri umuhimu wa One stop centre kuwa vituo hivyo vinasaidia kupatikana kwa wataalamu mbalimbali katika eneo moja, hivyo kumsaidia mhanga aliyefanyiwa ukatili kupata huduma stahiki kwa wakati na kwa muda mfupi kwani bila viuo hivyo mzunguko wake huwa ni mrefu jambo ambalo husababisha ushahidi wa matukio ya ukatili kupotea.
Mradi wa kizazi kipya unaofadhiriwa na USAID ulianza mwaka 2016 na unatarajia kuisha Mwaka huu.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.