Msemaji Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Gerson Msingwa amesema kumekuwa na ongezeko la ukusanyaji wa mapato katika sekta ya utalii kufikia trilioni 7.5 kwa mwaka 2023/2024 ambapo hapo awali mapato hayo yaliishia trilioni 2 hadi 3 pekee.
Msigwa amebainisha hayo Januari 25, Mwaka huu wakati akizungumza na waandishi wa habari ndani ya hifadhi ya Taifa ya Mikumi iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro.
Akifafanua zaidi, Msigwa amesema mapato hayo yametokana na ongezeko la watalii katika hifadhi za Taifa kutoka watalii 1,618,538 mwaka 2022/2023 hadi watalii 1,863,108 mwaka 2023/2024, hivyo kutokana na uwepo wa ubora wa miundombinu hususan barabara, Viwanja vya ndege na michezo na kumechochea ongezeko la mapato hapa nchini.
"...Mapato yetu yameongezeka sana sasa hivi tunazungumza mapato ya takribani trilioni 7.5 ambayo tumeyapata kupitia watalii wanaokuja kwenye hifadhi zetu..."
amesema Msigwa.
Aidha, Msigwa amesema Serikali imejipanga kukusanya kiasi cha Tsh. Bil. 430.9 Kupitia TANAPA katika mwaka wa fedha wa 2024/2025 lakini hadi kufikia Juni hadi Disemba zimekusanywa Tsh. bil. 325.1
Katika hatua nyingine, Gerson Msingwa amesema serikali imefanikiwa kutatua migogoro mbalimbali iliyokuwa ikiikumba sekta ya utalii ukiwemo mgogoro wa hifadhi ya Tarangire na kijiji cha Kimotoroki.
Migogoro mingine ni pamoja na ile ya hifadhi ya Serengeti na Vijiji saba vya Wilaya ya Serengeti, hifadhi ya Ruaha na Vijiji vya Mbalali, hifadhi ya Taifa ya Milima ya Mahale na Kijiji cha Kalilani huku serikali ikiendelea kuelimisha wananchi kuondokana na migogoro isiyo ya lazima kwenye maeneo ya hifadhi.
Sambamba na hayo, Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kusimamia na kuimarisha matumizi ya teknolojia katika kushughulikia shughuli za kihifadhi, ukusanyaji wa mapato, utangazaji wa utalii na fursa za nje ya nchi ili kukuza kipato cha Taifa.
Pia, Katibu Mkuu huyo amesema Serikali kupitia TANAPA imefanya uwekezaji na kuimarisha uhifadhi wa wanyama pori na makazi ya wanyama kwa kuimarisha ulinzi na usalama wa kiteknolojia na kufuatilia mienendo ya wanyama waliopo hatarini kutoweka wakiwemo Faru, Sokwe na Mbwamwitu ili rasilimali ziweze kuwa endelevu kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vizazi vijavyo.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.