Imeelezwa kuwa ulaji usiofaa wa vyakula na Mila potofu ni moja ya sababu zinazopelekea Mkoa wa Morogoro kuwa na hali duni ya lishe japo Mkoa huo ni miongoni mwa Mikoa inayozalisha chakula kwa wingi.
Hayo yamebainishwa Agosti 21, 2024 na Afisa Lishe wa Mkoa wa Morogoro Bi. Salome Magembe wakati wa kikao cha Tathmini cha Utekelezaji wa Mkataba wa Lishe kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Katika kikao hicho kilichokuwa na ajenda tatu muhim, kusoma taarifa na Maazimio ya kikao cha tarehe 25/7/2023, kuwasilisha mada kuhusu Utapiamlo na athari zake na kuwasilisha taarifa ya Tathmini ya Mkataba wa Lishe kwa mwaka wa Fedha 2023-2024 kilihusisha Wakuu wa Wilaya zote za Mkoa huo, Makatibu Tawala wa Wilaya, Wajumbe wa Sekretarieti ya Mkoa, Wakurugenzi wa Halmashauri, Wenyeviti wa Halmashauri, Maafisa Lishe pamoja na wajumbe wengine kutoka Halmashauri.
Taarifa iliyotolewa ilieleza hali halisi ya lishe ya Mkoa huo ikiwemo taarifa ya kiwango cha udumavu kwa watoto waliochini ya miaka mitano kuwa ni 30.6%, kiwango cha uzito pungufu kwa watoto waliochini ya miaka mitano kufikia 3.9%, pamoja na upungufu wa damu kwa watoto chini ya miaka mitano kuwa ni 68.1% hali iliyoibua baadhi ya wajumbe kutaka kujua sababu zinazopelekea hali hiyo.
Akibainisha sababu hizo Afisa Afya Mkoa wa Morogoro Bi. Salome Magembe amesema hali hiyo inatokana na sababu nyingi zikiwemo wakazi wa Mkoa huo kutozingatia ulaji wa vyakula mchanganyiko pamoja na kuendelea kufuata mila potofu ikiwemo ya baadhi ya wazazi kukatazwa kula baadhi ya vyakula hasa vyakula vya jamii ya wanyama.
”pamoja na kwamba Morogoro kuna mboga za majiani nyingi na matunda kwa kila msimu lakini bado jamii haina kasumba ya kutumia mboga za majani na matunda” amesema Bi Salome.
”kwenye sababu za msingi, kwa Morogoro ipo hii ya mila na desturi potofu kuna baadhi ya maeneo mzazi haruhusiwi kula baadhi ya vyakula hasa vyakula vya jamii ya wanyama” ameongeza Bi. Salome.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima ambaye alikuwa mwenyekiti wa Kikao hicho pamoja na mambo mengine alijikita kwenye utekelezaji wa Mkataba wa Lishe ambapo aliwaagiza Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Mkoa huo kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza afua za lishe kwa kila robo ya mwaka wa fedha badala ya kutoa fedha hizo wakati wa robo ya mwisho wa mwaka, hali inayozorotesha utekelezaji wa Mkataba huo.
Aidha, aliwataka watendaji hao kila mmoja kuhakikishe anatoa fedha zaidi ya shilingi 1,555 kwa kila mtoto aliye chini ya miaka mitano ndani ya Halmashauri yake kwa lengo la kufanikisha utekelezaji wa afua za lishe huku akiagiza Ajenda ya lishe iwe inajadiliwa kila vikao vya madiwani na vikao vya Kamati za Ulinzi na Usalama ngazi ya Wilaya.
Katika Hatua nyingine wajumbe wa kikao hicho walijadili kwa kina changamoto ya upatikanaji wa vitendea kazi, hususan Vibao vya kupimia urefu Watoto walio chini ya miaka mitano vinavyotumika kujua hali halisi ya udumavu wa watoto na azimio la kikao hicho likawataka Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa huo kununua vibao hivyo kabla au ifikapo Septemba 30, 2024.
Baadhi ya wajumbe kikao hicho akiwemo Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Best Magoma alishauri jambo la kupata vibao litiliwe mkazo huku Bw. Said Mwakapugi akiishauri Serikali ngazi ya Mkoa kama kuna uwezekano na inaruhusiwa kuzijengea uwezo taasisi ufundi zilizopo ndani ya Mkoa ili zitengeneza vibao hivyo badala ya kutegemea kutengenezwa sehemu moja pekee.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.