Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Ali Malima amesema ili Mkoa huo uweze kuyafikia mafanikio inahitaji Viongozi kuwa na umoja na mshikamano, sauti moja, uzalendo, upendo baina yao ili kuhakikisha kuwa wananchi wa Mkoa huo wanapata maendeleo.
Mhe. Adam Malima ameyasema hayo Oktoba 6 mwaka huu kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri cha Mkoa (RCC) kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa chuo cha ualimu cha Morogoro kilichopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema Mkoa wa Morogoro una fursa nyingi za kiuchumi kwenye kilimo, mifugo, na utalii ambazo zikiratibiwa na kusimamiwa vizuri Mkoa utapata mafanikio kuliko Mikoa mingine hapa nchini, hivyo amewataka viongozi hao kubadilisha mitazamo yao na kuupa kipaumbele Mkoa ili uweze kufanikiwa.
“...tunahitaji Morogoro tofauti, tunataka kuitoa Morogoro hapa ilipo sasa, tunahitaji kuibadilisha Morogoro bila kuchapana viboko aone tu kwamba ni sehemu ya majukumu yake...” amesema Mkuu wa Mkoa.
Aidha, Mhe. Malima ameziagiza Halmashauri za Mkoa huo kuendelea kusimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kufikia shilingi Bilioni 60 kwa mwaka wa fedha 2024/2025, hata hivyo amezitaka Halmashauri hizo kubainisha maeneo ya uwekezaji pamoja na kuboresha miundombinu ili kuvutia wawekezaji.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa amemkataa Meneja wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushindwa kusimamia miradi ya usambazaji umeme katika Vijiji vingi vya Mkoa huo huku akimrudisha makao makuu Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) wa Mkoa kwa kushindwa kuhudhuria bila sababu vikao muhimu vya kujadili masuala ya kimaendeleo ya Mkoa ambavyo vinalenga kutatua kero za wananchi.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Kilosa Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi ambaye pia ni mwenyekiti wa Wabunge Mkoani humo amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa nia yake njema ya kutaka Mkoa huo kufikia mafanikio yanayotarajiwa na wanamorogoro na watanznia wote huku akiwaomba viongozi kushirikana kubadilisha mitazamo ya wanamorogoro waweze kufikirie maendeleo zaidi.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mhe. Sebastian Waryuba ambaye pia ni mwenyekiti wa Wakuu wa wilya za mkoa huo kwa niaba ya Wakuu wa Wilaya wa Mkoa huo amemshukuru Mhe. Adam Malima kwa kuja na mipango thabiti ya kuuendeleza Mkoa huku akikiri kuwa watampa ushirikiano na kuyafanyia kazi maelekezo yaliyotolewa ili kufainikisha nia yake ya kuupatia maendeleo Mkoani huo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.