Wataalam wa masuala ya VVU na UKIMWI wamebainisha kuwa unyanyapaa kwa watu waishio na VVU ni miongoni mwa sababu zinazopelekea kuongezeka kwa maambukizi hayo, hivyo wameishauri jamii kuachana na tabia ya Kuwanyanyapaa watu waishio na VVU.
Hayo yamebainishwa Novemba 28, 2023 na Mratibu wa masuala ya Jinsia kutoka Tume ya Kudhibiti UKIMWI – TACAIDS Bi. Priscilla Nalitolela wakati wa mahojiano na mwandishi wa Habari hizi kwenye Kijiji cha Jamii ikiwa ni muendelezo wa Wiki ya Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani 2023.
Bi. Priscilla amesema kuwa unyanyapaa ni hali ya kumtenga mtu kutokana na hali yake kiuchumi, kiafya na kielimu. Aidha, ameongeza kuwa unyanyapaa kwa watu wenye VVU husababisha kuongezeka kwa maambukizi kwa sababu ya watu waishio na virusi wanakuwa wasiri kutowaambia watu wengine hali zao kuhofia kutengwa.
Mratibu huyo amebainisha madhara ya unyanyapaa yakiwemo kuharibu utaratibu wa dawa kwa watu waishio na VVU, kuongezeka kwa maambukizi kutokana na watu wenye VVU kuwa wasiri katika jamii.
Pamoja na madhara hayo Bi. Priscilla amesema unyanyapaa upo katika ngazi mbalimbali ikiwemo unyanyapaa binafsi, kaya/familia na unyanyapaa ndani ya jamii.
Katika hatua nyingine Bi. Priscilla ametoa wito kwa Vijana kujiamini kwenda kupima kujua hali zao za kiafya na kuanza kutumia dawa za kufubaza VVU – ARV kwa wale watakaobainika kuwa na maambukizi hayo.
Nao baadhi ya vijana waliotembelea na kupata elimu kwenye Kijiji hicho cha jamii akiwemo Bw. Kelvin Mrekoni amesema uwepo wa Kijiji cha Jamii kimemsaidia kufahamu mbinu mbalimbali za kudhibiti maambukizi ya VVU na UKIMWI katika jamii huku akiwashauri vijana wengine kuwa wawazi ili kudhibiti maambukizi mapya ya VVU na UKIMWI.
Bw. Lyassa Lyassa ni mmoja wa watu waishio na VVU ametumia fursa hiyo kuwashauri vijana kwenda kupima ili kubaini hali zao za kiafya kwa kufanya hivyo kutatimiza lengo la Serikali la kufikia Sifuri tatu ifikapo 2025 yaani kuwa na asilimia sifuri ya maambukizi mapya, kuwa na asilimia sifuri ya vifo vinavyotokana na VVU na UKIMWI na kuwa na asilimia sifuri ya unyanyapaa kwa watu waishio na VVU.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.