Upatikanaji wa mbegu bora za mazao ya alizeti na mchikichi na uwezeshaji wa wananchi katika kilimo cha mazao hayo kwa njia ya mikopo nafuu na ruzuku mbalimbali za pembejeo ni suluhisho la uhaba wa mafuta ya kula hapa nchini.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Kilimo na Umwagiliaji Hussein Bashe kupitia hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela katika ufunguzi wa mkutano wa wadau wa Sekta ya mafuta ya kula uliofanyika Mei 31 Mwaka huu katika Hoteli ya Morena iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Mkoani humo.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela akihutubia Mkutano wa Wadau wa Sekta ya mafuta ya kula hapa nchini Mei 31 Mwaka huu uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Moreni uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Martine Shigela amebainisha kuwa Serikali kwa kutambua uhaba wa mafuta ya kula hapa nchini, pamoja na kufanya jitihada mbalimbali ili upatikanaji wake uwe wa bei nafuu imeendelea kushawishi uwekezaji na wawekezaji katika kilimo cha michikichi na alizeti ili kufikia malengo hayo ya Taifa.
“Zao la alizeti ni miongoni mwa mazao ya kimkakati, kwa hiyo ni miongoni mwa mazao ambayo tukiwekeza vizuri tutaweza kufikia malengo tunayoyatarajia na ndio maana mwaka jana tumesambaza mbegu bure kwa wakulima wetu kama motisha” amebainisha Shigela.
Katika hatua nyingine kupitia Hotuba hiyo Mkuu huyo wa Mkoa ameweka wazi kuwa Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imetenga bajeti zaidi ya shilingi bilioni 150 kwa ajili ya pembejeo za ruzuku ili kufanikisha shughuli mbalimbali za kilimo cha mazao yakiwemo ufuta, alizeti na michikichi ili kuhakikisha changamoto ya mafuta ya kula inafikia mwisho.
Baadhi ya washiriki wa mkutano wa wadau wa Sekta ya mafuta ya kula hapa nchini wakishiriki ufunguzi wa mkutano huo uliofunguliwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela Mei 31 Mwaka huu katika ukumbi wa Hoteli ya Morena uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Aidha ndugu Beatus Malema ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi wa Uendelezaji mazao, masuala ya pembejeo na Ushirika kutoka Wizara ya Kilimo, amesema kuwa badala ya kutumia bilioni 400 kwa ajili ya kuagiza mafuta nje ya nchi ni vema kama taifa kwa kushirikiana na wadau kuendeleza kilimo cha zao la mchikichi na alizeti ili kuondoa kabisa tatizo la upatikanaji wa mafuta ya kula hapa nchini.
Kwa upande wake Bw. Henry Mariale ambaye ni Mwenyekiti wa chama cha wakulima wa zao la Alizeti ameiomba Serikali kusaidia mbegu bora za alizeti na zinazoweza kutosheleza kwa wakulima hao, ambapo kama chama wamejipanga kuleta hamasa kwa kila kaya wanaojihusisha na kilimo cha alizeti kulima heka mbili ili kuweza kusaidia upatikanaji endelevu wa mafuta yatokanayo na zao hilo hapa nchini.
Naye Bw. Ringo Ringo ambaye ni Mwenyekiti wa chama cha wasindika Mafuta Tanzania (TASUBA) amebainisha kuwa changamoto ya ukosefu wa mafuta hapa nchini umechagizwa kwa kiasi kikubwa na uhaba wa upatikanaji wa alizeti, kwani viwanda vya usindikaji vinapokea mali ghafi hiyo kwa uchache zaidi ukilinganisha na mahitaji halisi.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Mkutano wa wadau wa Sekta ya mafuta ya kula baada ya ufunguzi wa mkutano huo Mei 31 Mwaka huu katika ukumbi wa Hoteli ya Morena uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.