Imeelezwa kuwa utitiri wa Kodi kwa wafanyabiashara ni moja ya changamoto kubwa inayolalamikiwa na kundi hilo na kwamba jambo hilo si tu linadhohofisha maendeleo ya wafanyabiashara hao kuendesha biashara zao lakini pia linaikosesha Serikali kupata kodi inayostahili.
Hayo yamebainishwa Januari 22, 2025 na Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Maboresho ya kodi Balozi Mwanaid Maajar wakati wa kikao cha Tume hiyo kilichofanyika ukumbi wa mikutano wa Mbaraka Mwinshehe Manispaa ya Morogoro na kushirikisha wafanyabiashara mbalimbali wa kodi Mkoani humo kwa lengo la kukusanya maoni, changamoto na mapendekezo ili Serikali iweze kuboresha ukusanyaji wa kodi hizo.
Balozi Mwanaid amesema, kilio cha wengi ni utitiri wa kodi unaotokana na uchache wa walipa kodi huku Mamlaka husika zikiwa zinaelekeza nguvu zake za kudai kodi sehemu mojaama chache ili kupata kodi jambo ambalo linamrudisha nyuma mfanyabiashara kwa sababu ya kulipa kodi nyingi.
".. Utitiri wa kodi na watozaji wenyewe imejirudia mara nyingi kwamba wanafika watozaji wapatao hata wa tano kwa siku na bila mtu kujua.." amesema Balozi Mwanaid.
Katika hatua nyingine Balozi huyo ameeleza lengo la Tume hiyo kuwa imelenga kupokea malalamiko, changamoto na mapendekezo ili kuboresha mazingira ya kufanyia biashara na kuangalia namna ya kurahisisha utaratibu wa wafanyabiashara kupata leseni, kulipa tozo na kulipa kodi kwa urahisi.
Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mkoa wa Morogoro Bi. Beatrice Njawa amesema katika eneo muhimu sana katika kuboresha mazingira ya biashara hapa Nchini ni kuangalia suala la wingi wa kodi ambalo linaweza kuwavutia wawekezaji wengi, hivyo ameiomba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kushirikiana katika kutoa mafunzo kwa wafanyabiashara juu ya umuhimu wa kulipa kodi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara na Kilimo Mkoa wa Morogoro (TCIA) Mwadhine Mnyanza amesema wafanyabiashara hukumbana na changamoto mbalimbali zikiwemo wingi wa kodi, kodi kubwa hasa katika sekta zinazokuwa kibiashara jambo linalopelekea wafanyabiashara kufikia hatua ya kukwepa kodi.
Naye Katibu wa Chama Cha Walimu (WCT) manispaa ya morogoro Bw. George Lukoa amesema, moja ya kero kubwa wanayokumbana nayo wafanyakazi wa Umma hususan Walimu ni juu ya kodi ya makato (pay as you earn) kuwa kubwa jambo ambalo linapelekea mtumishi huyo kupata mshahara mdogo usiokidhi mahitaji hivyo ameiomba Serikali kuangalia upya suala hilo ili kupunguza kodi hiyo.
Katika hatua nyingine Bi. Redempta Mushi akieleza changamoto wanayokumbana nayo pindi wanapofanya biashara zao Zanzibar amesema, Mfanyabiashara kutoka Tanzania bara anatakiwa alipe kodi anapopeleka biashara zake zanzibar lakini mfanyabiashara kutoka Zanzibar halipi kodi jambo ambalo amesema inafaa liangaliwe ili kuweka uwiano kwa pande hizo mbili.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Ifakara Bi. Zahara Michuzi ameunga mkono hoja ya Serikali kuangalia kwa jicho la huruma mishahara ya wafanyakazi kwani amesema makato ni makubwa mno na mishahara haiongezeki jambo ambalo linapelekea umasikini kwa watumishi hao.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.