Kamishna wa Operation na Mafunzo Jeshi la Polisi Tanzania CP, Awadhi Juma amesema uzembe wa dereva wa gari la mizigo kwa kutofuata sheria na kanuni za barabarani ndio chanzo cha ajali iliyopelekea vifo vya watu 15 na kujeruhi watu 7 katika eneo la Mikese barabara ya Morogoro - Dar es Salaam.
CP. Awadhi Juma amebainisha hayo Disemba 18, 2024 wakati akiwa eneo la tukio la ajali iliyotokea Disemba 17, 2024 iliyohusisha gari la mizigo na gari ya abiria kugongana uso kwa uso majira ya saa 2 usiku Kata ya Mikese Mkoani Morogoro.
Kamishna wa polisi amesema dereva wa gari hilo hakufuata sheria, taratibu na kanuni za barabarani kwa kujaribu kuyapita magari mengine bila kujali watumiaji wengine wa barabara.
".. chanzo cha ajali hii inaonyesha kwamba ni uzembe wa dereva wa lori ambaye alikuwa anatokea Dar es Salaam kuelekea Morogoro kwa kutaka kuyapita magari ya mbele yake bila kuwa na tahadhari yoyote" amesema CP Awadhi.
Aidha CP. Awadhi amesema Jeshi la polisi halitasita kuwachukulia hatua Madereva wazembe wanaosababisha ajali barabarani na kutoa wito kwa madereva wote nchini kuzingatia sheria za barabarani ili kuweza kupunguza ajali pia jeshi hilo limetoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki kwa kupoteza wapendwa wao katika ajali hiyo.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro Dkt. Daniel Nkungu amesema hadi kufika leo Disemba 18, 2024 Jumla ya watu waliofariki kwenye ajali hiyo ni 15 na majeruhi 7 huku hali za majeruhi hao zikiendelea vizuri kwa kupatiwa matibabu katika Hospitali hiyo.
Pia amesema Hadi kufikia leo Disemba 18, 2024 miili ya watu watano kati ya 15 tayari ilikuwa imetambuliwa na ndugu zao, huku zoezi la kutambua miili iliyobaki likiendelea kwa siku 14 na baada ya muda huo ambao watakuwa hawajatambuliwa, hatua za kuwasitiri wapendwa hao litafanyika kwa mujibu wa taratibu za kiserikali.
Katika ajali hiyo madereva wote wawili walifariki dunia.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.