Vijana Mkoani Morogoro wanatarajia kunufaika kupata masomo ya Elimu ya Sekondari huria (QT) na mafunzo ya ufundi stadi kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 kwa ufadhili kutoka Serikali ya Watu wa Marekani kupitia Mradi wa USAID KIJANA NAHODHA.
Kwa mujibu wa Meneja wa Mradi wa USAID KIJANA NAHODHA Bw. Samuel Chambi, amesema ufadhili huo kwa vijana watakao kidhi vigezo vilivyowekwa utajumuisha ada, chakula na usafiri kwa vijana wenye umri kuanzia miaka 15 hadi 25.
habari hiyo njema kwa vijana imebainishwa wakati wa mafunzo ya uhamasishaji wa mradi huo ngazi ya jamii Mkoani Morogoro yaliyotolewa kwa Halmashauri mbili za Morogoro DC na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Mafunzo hayo ya kutambulisha mradi huo yametolewa kwa Wadau mbalimbali wakiwemo Wahe. Madiwani wa kutoka kata zilizochaguliwa kunufaika na mradi huo kwa awamu hii ya kwanza, Maafisa elimu wa Kata husika pamoja na Maafisa Maendeleo ya Jamii wa halmashauri nufaika.
Akifungua mafunzo hayo kwa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Aprili 14 mwaka huu katika hoteli ya Flomi, Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Mhe. Pascal Kihanga amekiri kuwa kuanzishwa kwa mradi wa USAID KIJANA NAHODHA katika Manispaa hiyo utasaidia vijana wengi kujikwamua katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
Wakizungumzia manufaa ya mradi huo siku ya kwanza ya kuutambulisha, wajumbe wa mafunzo hayo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro akiwemo Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mhe. Lucas Lemomo amesema itawarahisishia wasichana na wavulana ambao walikatisha masomo yao kwa sababu mbalimbali kuendelea na masomo huku wakiendelea na shughuli zao nyingine za Uzalishaji.
Ameongeza kuwa mradi huo utawasaidia vijana hao kupata ujuzi lakini zaidi kufikia malengo yao ambayo walishakata tamaa kuyafikia.
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri hiyo Bi. Frola Mwambele amesema mafunzo hayo yatawafikia vijana wengi ambao awali walikuwa hawapati fursa ya kufikiwa na miradi mbalimbali hivyo ni fursa kwa kwao kubadilisha maisha kupitia mradi huo.
Mradi huo wa miaka mitano ambao ulianza Septemba 2022 na utakamilika 2026 unatekelezwa kwa Mikoa yote ya Tanzania Visiwani na kwa Tanzania Bara utatekelezwa kwa mikoa miwili ya Morogoro na Dar es salaam ukilenga kuwafikia na kuwanufaisha jumla ya vijana 45,000 wa kutoka Maeneo hayo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.