Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela amewataka vijana kutoka katika Halmashauri za Mkoa huo na maeneo jirani kujitokeza na kujiunga kwenye mradi wa Vijana unaojulikana kama Kizimba Business Model, unaojikita katika kilimo cha Bustani na Mbogamboga.
Martine Shigela ametoa rai hiyo Agosti 12 mwaka huu alipotembelea shamba lenye ukubwa wa ekari 1,500 ambalo lipo Wami Luhindo Wilayani Mvomero lililoanzishwa na Ushirika wa Wajasiliamali waliohitimu Chuo Kikuu cha Sokoine (Sokoine University Graduate Entrepreneurs Cooperative – SUGECO) kwa lengo la kuwajengea Vijana kushiriki kujenga uchumi wao na Taifa kupitia kilimo.
Amesema, Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejikita katika uzalishaji, na SUGECO, UNDP pamoja na baadhi ya Taasisi za kibenki hapa nchini ziko pamoja katika kutekeleza dhamira hiyo ya Rais kupitia mradi huo, hivyo amewataka vijana kuitikia wito wa kwenda kufanya kazi kwa bidii kwenye mradi huo ili kupata tija.
“kwa hiyo kazi yenu sasa kama vijana ambao mtakaokuja hapa ni kuweka jitiahada kwa kuweka nguvu kubwa katika uzalishaji wa haya mashamba” ameshauri Martine Shigela.
Naye Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa (UNDP) hapa nchini Bi. Chritina amesema UNDP imefurahishwa na mradi huo na wako tayari kushirikiana katika kuwasaidia vijana kushiriki mradi huo wa kilimo na kuwafanya wakipende kilimo kwa kuwa kinaweza kuwapatia fedha za kutoshereza mahitaji yao hivyo kupunguza vijana wasio na kazi na kuzurura mitaani huku akiwataka vijana wasichana kuchangamkia fursa hiyo.
Katika hatua nyingine mwakilishi huyo wa UNDP amebainisha kuwa vijana watakaopatikana watapelekwa katika mafunzo ya kilimo hicho nchini Israel na baada ya kipindi cha miezi 11 watarudi hapa nchini na kuanza kazi hiyo ya kulima mazao ya mbogamboga.
Awali akimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kuzungumzia ziara hiyo, mara baada ya kutembelea mradi huo, Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Halima Okash ambako mradi huo upo, pamoja na kuishukuru SUGECO kuwapelekea mradi huo Wilayani kwake, amesema mradi huo unakwenda kutatua changamoto ya vijana wengi kukosa ajira na kuwataka vijana wenye sifa kuchangamkia fursa hiyo.
Akitoa taarifa ya Mradi huo wa Vijana unaojulikana kama Kizimba Business Model, Mkurugenzi wa SUGECO (Sokoine University Graduate Entrepreneurs Cooperative) Revocatus Kimario amesema lengo la mradi huo ni kuwainua vijana kiuchumi kwa kujiajiri katika kilimo hicho cha biashara na chenye uhakika wa soko la mazao yote yatakayolimwa hapo.
Ameongeza kuwa mazao yatakayolimwa ni yale ya bustani na mbogamboga ambayo tayari yamekwisha tafutiwa masoko na kwamba tija ya kupata Tsh. laki tano kwa mwezi huku akitoa wito kwa Halmashauri zitakazokuwa tayari kutoa ardhi zitapelekewa mradi huo ili ziweze kuongeza mapato yatokanayo na mradi huo.
Kwa upande wa Taasisi za Kibenki ambazo zimeunganishwa kwenye mradi huo, Graison Fednand ambaye ni Afisa kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADM) kwa niaba ya Taasisi nyingine za Kibenki amesema changamoto waliyokuwa wakiipata katika kutekeleza jukumu lao la kutoa mikopo kwa vijana ni ugumu wa kuwakusanya pamoja, hivyo hiyo itakuwa fursa kwao kutoa mikopo kwa vijana watakaojiunga na mradi na kushirikiana na viongozi wengine wa mradi huo ili uweze kufanikiwa.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa SUGECO Dkt. Anna Temu ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoinne ameeleza kuwa SUGECO imeanza tangu mwaka 2011 kwa lengo la kuwawekea mazingira mazuri wahitimu wa chuo hicho na wengine wanaotaka kuwa wawekezaji wakubwa katika sekta ya Kilimo kwa kuwaondolea changamoto za sekta hiyo na kutimiza ndoto zao.
Mradi huo unatarajiwa kuanza na vijana 500 katika utekelezaji wake ambapo vigezo vya kujiunga katika mradi huo ni lazima vijana wawe na Stashahada au Shahada ya kilimo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.