Wito umetolewa kwa vijana wa umri wa kati ya miaka 15 hadi 24 kujitokeza kwa wingi kupima afya zao ili kukabiliana na ongezeko la maambukizi ya Virusi vya UKIMWI na VVU hapa nchini
Wito huo umetolewa Novemba 26 mwaka huu na Naibu Waziri wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye ulemavu Mhe. Patrobas Katambi kwenye kongamano la Vijana la Kisayansi lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Morena.
Mhe. Patrobas Katambi amesema kuwa utafiti wa viashiria vya UKIMWI nchini uliofanyika 2016/2017 unaonesha kuwa kundi la vijana walio kati ya umri wa miaka 15 hadi 24 hawajui hali zao za maambukizi ukilinganisha na makundi mengine hususan kundi la watu wazima.
“...natoa rai kwa vijana wote nchini kujitokeza kwa wingi katika huduma za upimaji VVU kwa hiari zinazotolewa sehemu mbalimbali hapa nchini...” amesema Naibu Waziri Patrobas Katambi.
Aidha, amesema kuwa katika kuelekea lengo la sifuri ya maambukizi mapya, kutokana na jitihada mbalimbali za mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI, maambukizi mapya yameendelea kushuka mwaka hadi mwaka ambapo watu 54000 waliambukizwa VVU mwaka 2021.
Sambamba na hilo, Naibu Wazri huyo amewaasa vijana kuwa na mitazamo chanya na kuwa na malengo madhubuti ya kufanya mambo kulingana na mazingira na jamii wanamoishi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Vijana Wanaoishi na VVU Bi. Pudensia Mbwiliza amesema nguvu kubwa inahitajika kuwasukuma Vijana ili waweze kubadilika kutokana na kuwa na mwitikio mdogo kwenye masuala ya VVU na UKIMWI huku akiwaasa vijana kushikamana ili kuhakikisha kuwa wanabadilika kwa lengo la kudhibiti maambukizi mapya ya VVU na UKIMWI.
Naye mwakilishi wa Shirika la Kimataifa la kudhibiti UKIMWI - UNAIDS Bi. Grace Mallya amesema mkakati wa kidunia wa kumaliza maambukizi ya UKIMWI ifikapo 2025 umeainisha kuwa asilimia 30 ya huduma zote za upimaji na tiba zifanywe na Vijana kutokana na kundi hilo kuwa na idadi kubwa ya maambukizi mapya ya VVU, hivyo ametoa wito kwa wadau wa maendeleo kwa kushirikiana na Serikali kuwajengea uwezo Vijana ili kufikia malengo ya kumaliza maambukizi ya VVU na UKIMWI duniani.
Kongamalo hilo la Vijana la Kisayansi limewakutanisha vijana kutoka Vyuo vikuu, vya kati na Sekondari likilenga kubadilishana uzoefu na kupata uelewa juu ya kudhibiti na kujikinga maambukizi ya VVU na UKIMWI.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.