Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanikiwa kuwapelekea umeme wananchi wa Vijiji 652 kati ya vijiji 669 vya Mkoa wa Morogoro kupitia Wakala wa Nishati ya Umeme Vijijini (REA) huku ikiahadi kukamilisha kupeleka nishati hiyo kwa vijiji 17 vilivyobaki ndani ya wiki tatu zijazo.
Hayo yamebainishwa Oktoba 4, Mwaka huu na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima wakati wa kikao na viongozi wa REA kilichofanyika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo kikiwa na lengo la kutathmini hatua za mradi ulipofikia na kumtambulisha mkandarasi mpya wa kampuni ya SINOTEC CO. LTD.
Akifafanua zaidi, Mhe. Malima amesema, Mkoa huo una vijiji 669 ambapo vijiji vilivyofikiwa na nishati ya umeme ni 652 sawa na asilimia 97.5 huku vijiji 17 vilivyobaki vikiwa kwenye hatua za mwisho za ukamilishaji na kwamba vijiji hivyo vinatarajiwa kukamilika kupata umeme ifikapo mwezi Oktoba mwaka huu.
“…nasema Morogoro ina vijiji 669 vilivyofikiwa katika kipindi hiki ni vijiji 652 sawa na asilimia 97.5 huo ndio ukweli…” amesema Mhe. Adam Kighoma malima
Kutokana na mafanikio hayo, kiongozi huyo amesema, kwa sasa REA wameelekeza nguvu zao katika kuvipatia nishati ya umeme vitongoji 3,369 vya Mkoa huo huku vitongoji 1,655 tayari vimekwishapatiwa umeme sawa na asilimia 49.
Aidha, amesema vitongoji 455 vinatarajiwa kupatiwa umeme kwa kipindi cha miaka miwili na ndani ya hivyo vitongoji 289 mkandarasi anaendelea na ujenzi kupitia mradi wa ujazilizi (Densification IIB) na vitongoji 166 vitapatiwa umeme kupitia mkandarasi mpya aliyetambulishwa leo Oktoba 4, 2024.
Mhe. Malima ametumia fursa hiyo kuipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kuiwezesha REA kufanikisha mradi huo wa umeme ulioanza kutekelezwa kwa shilingi Bil. 2 pekee mwaka 2008 kwa nchi nzima na sasa serikali inatoa shilingi Bil. 154 kwa Mkoa huo pekee hivyo kuleta ufanisi kwa sekta nyingine za kijamii kama Elimu, Afya, na hata nyumba za ibada.
Sambamba na pongezi hizo, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wadau mbalimbali wakiwemo wenyeviti wa vijiji na vitongoji, watendaji wa kata na viongozi wengine kutoa ushirikiano wa kutosha kwa mkandarasi huyo ili kurahisisha utekelezaji wa mradi wenyewe.
Kwa upande wake, Mhandisi Mkuu wa Mkoa huo, Mhandisi Adam Abdulla kwa niaba ya Meneja wa TANESCO Mkoa wa Morogoro ameishukuru serikali kwa kutoa fedha kwa ajili ya mradi huo na kuahidi kuusimamia na kutoa ushirikiano kwa mkandarasi ili akamilishe kazi hiyo kwa wakati.
Naye, Msimamizi wa Miradi Kanda ya Kati Mhandisi Aneth Malingumu amesema, mradi huo ni maalum kwa kuwa usanifu wake umefanyika kupitia majimbo yote 11 ya Mkoa huo na kila jimbo litapata umeme katika vitongoji 15 likiwemo jimbo la Morogoro Mjini.
Mradi huu wa kufikisha nishati ya umeme vijijini unatekelezwa ndani ya miezi 24 na mkandarasi atakayesimamia ni kutoka kampuni ya SINOTEC CO. LTD ambaye ametambulishwa leo Oktoba 4, Mwaka huu.
Mwisho
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.