Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwassa amewataka Viongozi wa dini katika Mkoa huo kuwa mabalozi wa amani kwa kuwa wao wanaushawishi na nguvu kubwa katika kuwabadilisha waumini wao kitabia kupitia mafundisho wanayoyatoa kwenye nyumba zao za ibada.
Mhe. Fatma Mwassa ametoa kauli hiyo Novemba 16 mwaka huu wakati akifungua kikao cha kawaida cha Kamati ya Afya ya Msingi kwa Jamii kilichohusisha wataalamu wa Sekta ya Afya Pamoja na Viongozi mbalimbali wa dini Mkoani humo.
Mhe. Fatma Abubakar Mwassa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro akifungua kikao hicho.
Mhe. Fatma Mwassa amewaomba viongozi hao wa dini kutoa Elimu kwa waumini wao kuacha kujichukulia Sheria mikononi lakini pia kutoa taarifa kwa mamlaka husika pindi wanapoona kuna uvunjifu wa amani, ukiukwaji wa Sheria, taratibu na kanuni Katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za uingizaji wa makundi makubwa ya mifugo unaendelea sasa Mkoani humo jambo ambalo amesema linachangia uvunjifu wa amani.
Baadhi ya Viongozi wa Dini walioshiriki kikao cha Afya ya Msingi
“...kwahiyo tunawaomba leo viongozi wetu wa dini, tunajua nyinyi mnanguvu kubwa na maneno yenu yanaushawishi mkubwa, tunaomba mkatusaidie kuelimsha jamii...” amesema Mhe. Fatma Mwassa.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa, amewataka viongozi hao kutoa Elimu kwa waumini wao juu ya mabadiliko ya tabia nchi yanayosababisha ukame katika maeneo mengi hapa nchini na duniani kwa ujumla na kwqmba hali hiyo imechangiwa vikubwa na shughuli za kibinadam kama ukataji miti hovyo, uchomaji moto misitu, kuharibu vyanzo vya maji na shughuli nyingine zinazofanana na hizo, na kutaka kuwa mabalozi wazuri kukemea matendo hayo.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dr. Mussa Ali Mussa akiongea na viongozi wa dini na wajumbe wa kamati ya Afya ya Msingi ya Jamii waliohudhuria kikao hicho.
Aidha, ametumia fursa hiyo kuwataka viongozi wa dini kuelimisha waumini wao kupata chanjo ya uhonjwa wa Uviko 19 na chanjo za magonjwa mengine Kama surua na polio ili kuiweka jamii salama kiafya.
Kwa upande wake Shekhe mkuu wa Mkoa wa Morogoro Shekhe Twaha Kilango ameshauri viongozi wa Serikali kutumia zaidi busara zao Katika kutatua migongano ndani ya jamii ikiwemo Ile ya baina ya wakulima na wafugaji, kwa kuwa nguvu pekee inaweza kuleta madhara makubwa lakini pia isilete Suluhu ya kudumu ya tatizo husika.
Sambamba na ushauri huo amewataka viongozi wenzake wa dini kuwa mstari wa mbele katika kuwaelimisha waumini juu ya masuala ya amani na na masuala ya afya.
Naye Mhasham Askofu Jacob Mameo wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania - KKKT Dayosisi ya Mashariki amesema wapo tayari kwenda kukutana na makundi yote mawili ya jamii ya wafugaji na wakulima kwa lengo la kuwatuliza waache vurugu ambazo uwenda zinasababisha balaa la kutonyesha kwa mvua na mabalaa mengine.
Baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dr. Kusirye Ukio
Akitoa tathmini ya utoaji wa chanjo ya ugonjwa wa UVIKO - 19 Mkoani humo Mratibu wa Chanjo Mkoa wa Morogoro Dkt. Masumbuko Igembye amesema toka Agosti 2, 2021, hadi Oktoba 31, 2022, takribani watu 1,022,093 sawa na 66.2% wamechanjwa kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo huku lengo likiwa ni kutoa chanjo kwa watu 1,544,177 Mkoani humo.
Aidha, Dkt. Masumbuko amewataka viongozi wa dini kuwahamasisha waumini wao kuchanja ili kufikia lengo la asilimia 80 hali itakayoleta matumaini ya mkoa huo kuwa salama dhidi ya ugonjwa wa COVID - 19.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.