Viongozi wa Dini wametakiwa kutumia majukwaa hayo kutoa elimu kwa jamii kuwa na mwitikio chanya katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI kwa kuwa wao wana ushawishi katika mkubwa kwa jamii zao.
Nasaha hizo zimetolewa leo Novemba 29, 2023 na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi wakati akifungua mdahalo wa Vijana na Viongozi wa Dini uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Nashera iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Dkt. Yonazi amesema kuwa Viongozi wa Dini wanaushawishi mkubwa katika jamii zao hivyo wanatakiwa watoe elimu kwa waumini wao kupitia nyumba hizo za ibada kwani kwa kufanya hivyo jamii itakuwa na mwitikio chanya juu ya mapambano dhidi ya UKIMWI na kuisaidia jamii kuwa na uelewa wa masuala ya UKIMWI.
“...nitoe rai kwa viongozi wa dini kutumia majukwaa yao kutoa elimu ili kusaidia kuhamasisha waumini na jamii ambayo ni vijana, watoto na watu wazima kuwa na mwitikio uliyochanya dhidi ya mapambano ya UKIMWI...” amesema Katibu Mkuu.
Aidha, Katibu Mkuu huyo amebainisha kuwa kupitia elimu hiyo itawezesha nchi kufikia malengo ya 95 tatu ifikapo 2025 dhidi ya mapambano ya ugonjwa wa UKIMWI yaani asilimia 95 ya watu wawe wanajua hali zao, asilimia 95 ya watu wanaotumia dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI – ARV na asilimia 95 ya tatu watu wanaotumia dawa za ARV wawe wamefubaza virusi hiyo.
Katika hatua nyingine Dkt. Jim Yonazi amewashauri wadau wanaotekeleza afua za UKIMWI nchini kuwajengea uwezo Viongozi wa dini kuhusu elimu ya VVU na UKIMWI, ukatili wa kijinsia, elimu ya Afya ya uzazi, unyanyapaa na ubaguzi, mimba na ndoa katika umri mdogo hii itasaidia kuongeza ushiriki wa Viongozi hao katika mapambano ya dhidi ya UKIMWI.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano Mkoa wa Morogoro Shekhe Juma Yahaya ametumia mdahalo huo kuwakumbusha Vijana kuwa ni Taifa la Kesho hivyo amewataka kujikinga na maambukizi ya VVU pamoja na kuwashauri Vijana waliopo katika ndoa kuheshimu ndoa zao huku akisisitiza vijana kufuata maamrisho ya dini zao.
Naye Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya Dkt. Catherine Joakim amewashukuru Viongozi wa dini kwa niaba ya Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu kwa kuwa viongozi hao wamekuwa na mchango mkubwa katika kufikisha elimu ya masuala ya Afya kwa waumini wao hususan mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.