Chama cha Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini - TAGCO kimewataka Maafisa habari hapa nchini kuiga mfano wa vitengo vya habari vinavyofanya vizuri katika utekelezaji wa majukumu yao kikiwemo Kitengo cha Habari cha Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Mkoani humo ikiwa ni pamoja na kuwahabarisha wananchi juu ya shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hayo yameelezwa na Mjumbe Mtendaji wa TAGCO Bw. Karim Meshack Agosti 30 mwaka huu kwa niaba ya Wajumbe wenzake wakati wa ziara ya Uongozi wa Chama hicho wakishirikiana na Maafisa Habari Waandamizi kutoka Idara ya Habari Maelezo walipotembelea Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Baadhi ya Viongozi wa TAGCO waliofanya ziara Mkoani Morogoro. kutoka kushoto ni Karim Meshack, Gerlad Chami ambaye alikuwa Mkuu wa Msafara katika ziara hiyo na Fred Mwanjala ambaye pia ni Afisa Habari Mwandamizi Idara ya Habari Maelezo.
Bw. Gerlad Chami akiwasilisha ujumbe wa TAGCO kwa Kaimu Mkurugezi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro wakati wa kikao
Bw. Meshack amebainisha kuwa, katika Halmashauri zote za Mkoa wa Mkoa huo, Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ndiyo imekidhi hadhi ya kuwa kitengo cha habari katika utekelezaji wa majukumu yake kutokana na Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo kumwezesha Afisa habari kuwa na Maafisa habari wasaidizi watano ambao wanasaidia kuwapasha habari wananchi kwa wakati.
‘’Kitu kikubwa zaidi ambacho kimetufurahisha katika Manispaa ya Morogoro ni Mkurugenzi kumuwezesha Afisa habari kuwa na Maafisa wengine wa habari watano ili kuhakikisha taarifa za utendaji kazi za Manispaa zinawafikia wananchi kwa wakati’’ amesema Meshack.
‘’kazi nyingi zinafanyika vizuri za kutangaza Manispaa na Mkoa kwa ujumla kutokana na uwepo wa Maafisa habari wa kutosha, tunaona namna ambavyo wanauza vivutio vilivyomo katika manispaa ya Morogoro ikiwemo stendi ya kisasa, soko, water falls na mambo mengine’’ ameongezea Meshack.
Katika hatua nyingine, Meshack amebainisha kuwa Maafisa habari wa taasisi ni wasemaji na wawakilishi wa Msemaji Mkuu wa Serikali na Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo katika kufikisha taarifa mbalimbali zinazotekelezwa katika Halmashauri au Mkoa husika.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya morogoro Bi. Pilly Kitwana, pamoja na kushukuru ujio wa Viongozi wa Chama cha Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini-TAGCO, amesema ujio wao umesaidia kutambua mapungufu machache waliyo nayo hususan ya kutomtumia vyema Afisa Habari wa Halmashauri hiyo.
Aidha, ametumia fursa hiyo kumtaka Afisa Habari wa Halmashauri kuongeza juhudi katika kutangaza kazi zinazofanywa na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro na Serikali kwa ujumla pamoja na kutangaza vivutio vyote vinavyopatikana ndani ya Halmashauri ya Manisapaa ya Morogoro.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Pilly Kitwana
Kwa upande wake Afisa habari wa Mkoa wa Morogoro Ndg. Andrew Chimesela amesema ujio wa TAGCO katika Mkoa huo umelenga kutathmini utendaji kazi wa Maafisa habari, kutoa ushauri na kuangalia namna ya kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili Maafisa Habari wa Halmashauri za Mkoa huo.
Aidha, Bw. Chimesela amewapongeza Viongozi wa TAGCO kwa kuanzisha utaratibu wa kuwatembelea Maafisa wa habari kwa lengo la kujua changamoto zao na kuzitatua jambo ambalo amesema utamaduni huo unafaa uendelee ili kuleta mafanikio chanya ya Tasnaia ya Habari.
Naye, Afisa habari wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Bi. Lilian Henry licha ya kuipongeza TAGCO, amesema ziara hiyo ya Wajumbe wa chama cha TAGCO imewatia moyo katika kukabiliana na changamoto ambazo Maafisa habari wanakumbana nazo hivyo kuwajengea uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi.
Lilian Henry Afisa Habari Manispaa ya Morogoro
Mkuu wa Kitengo cha ICT Manispaa ya Morogoro, Bw. Kitutu Mshana
MWISHO.
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.