Wajumbe wa kamati ya uongozi wa Taifa wa mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) wameridhika na utendaji kazi wa mradi wa mfuko huo na kuwataka viongozi wa TASAF kutoa taarifa sahihi na kwa wakati kwa wananchi ili kuepuka fikra ambazo zinakwamisha maendeleo ya wananchi.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Maghembe akizungumza na wananchi.
Kauli hiyo imetolewa Julai 28, 2023 na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Maghembe wakati akiwa kwenye ziara yake ya siku moja pamoja na wajumbe wa kamati ya Uongozi wa Taifa wa TASAF walipotembelea Kijiji cha Bamba kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Mkoani Morogoro ikiwa na lengo la kuona jamii inavyonufaika na mradi huo.
Dkt. Maghembe ametoa kauli hiyo wakati akitoa ufafanuzi wa malalamiko kutoka kwa wanufaika wa mradi huo, baadhi ya malalamiko hayo ni pamoja na kutopewa taarifa sahihi na kwa wakati ya kununuliwa vifaa vya kusafishia barabara vikiwemo majembe ilihali vifaa hivyo tayari vilikuwa vimekwisha nunuliwa kwa ajili ya jamii hiyo.
Sambamba na hilo Dkt. Maghembe amewataka wananchi kutumia vizuri vifaa hivyo ili kupunguza gharama za uendeshaji wa mradi huo na kupanua wigo wa kutoa huduma kwa wananchi.
"... Kwa hiyo niombe sana TASAF pamoja na Viongozi wote wa serikali za mitaa mliopo hapa tuwe na mawasiliano mazuri na wananchi kwani tunavyo vikao vyetu vya ngazi ya kitongoji, Kijiji, kata, kamati za Afya na kamati za mazingira, tuvitumie kuwapa taarifa sahihi wananchi..." Amesema Dkt. Magembe.
Aidha, Dkt. Maghembe ameongeza kuwa Viongozi hao wanatakiwa kushirikiana na wananchi ili kuwaweka karibu na miradi ya maendeleo, hata hivyo amesema vikao vinavyofanyika vikiwemo vikao vya ngazi ya vitongoji, vijiji, Kamati za Afya, kamati za mazingira n.k. hivyo ni vikao vinavyotakiwa kutumika kutoa taarifa sahihi na kwa wakati kwa wananchi.
Katika hatua nyingine, Dkt. Maghembe amemuagiza Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Bi. Florence Mwaribewe kufanya marekebisho na kuongeza baadhi ya huduma zitakazotolewa katika kituo cha Afya cha Bamba ili kitoe huduma za uhakika kwa wananchi.
Pichani ni Naibu Katibu Mkuu wa miundombinu TAMISEMI Mhandisi Rogatus Mativila akifafanua jambo wakati wa mkutano na wananchi.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa miundombinu TAMISEMI Mhandisi Rogatus Mativila amesema barabara inayounganisha Kijiji cha Bamba na Morogoro Manispaa ambayo haikutengenezwa itapewa kipaumbele katika bajeti ya mwaka wa Fedha 2023/2024 kuhakikisha inakamilika ili kuondoa changamoto ya kuchelewesha wagonjwa kuwahi kupata huduma za Afya sambamba na watoto wa shule kuwahi shuleni.
Nao wanufaika wa Mradi huo akiwemo Bi. Habiba Abedi wa Kijiji cha Bamba ameushukuru uongozi wa mradi huo kwa kuwasaidia wananchi kwani umebadilisha maisha ya wanufaika kwa kuwawezesha kununua mifugo kama vile mbuzi, kuku, ng'ombe n.k. pamoja na kununua sare za watoto.
Baadhi ya wananchi waliojitokeza kwenye mkutano.
Hivyo, wananchi hao wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa na Viongozi wanaouendeleza vema mradi huo na kuwafikia wananchi wa hali ya chini.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilianza kutekeleza mradi wa Mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) kuanzia mwaka 2000, ikiwa na lengo la kunusuru kaya masikini hapa nchini.
Bw. Jacob Kayange kwa niaba ya Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Mipango na Uratibu akizungumza na wananchi waliojitokeza kwenye mkutano.
Mwisho
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.