Viongozi na wanachama wa vyama vya ushirika Mkoani Morogoro wameaswa kuondokana na tabia ya kutolipa madeni ya mikopo yao kwa wakati kwani kufanya hivyo kunapelekea kutostawisha vema mitaji ya vyama hivyo na kupelekea kuwa tegemezi.
Hayo yamebainishwa Juni 21 kupitia hotuba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela iliyosomwa kwa niaba yake na Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Mhe. Pascal Kihanga wakati wa kufunga maadhimisho ya Jukwaa la vyama vya ushirika Mkoani humo yaliyofanyika katika ukumbi wa Savoy katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Mhe. Pascal Kihanga akizungumza na maafisa ushirika alipomwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela wakati wa kufunga jukwaa la ushirika Mkoani humo Juni 21 mwaka huu.
Aidha, Mhe. Mstahiki Meya huyo amesema kuwa taasisi za mabenki pamoja na Sacoos za ushirika zinajiendesha kwa faida ambapo hutegemea mnyororo wa kukopa na kurudisha fedha kwa wakati hivyo kuchelewa kurejesha fedha hizo ni kukwamisha shughuli za taasisi na Saccos husika.
“Niwaagize viongozi na wanachama wote waliopo katika ukumbi huu kuhakikisha mnaacha tabia ya kutolipa madeni kwa wakati,hivyo ni kuchelewa kustawisha na kuongeza mitaji yenu” amesema Mhe. Mstahiki Meya.
Katika hatua nyingine Pascal Kihanga amewataka viongozi na mamlaka zinazosimamia vyama vya Ushirika Mkoani Morogoro kuongeza kasi ya kukagua na kusimamia kwa ukaribu na kuchukua hatua za haraka pindi inapoonekana Kuna taarifa za ukiukwaji wa sheria na miongozo ya vyama hivyo vya ushirika.
Kwa upande wake Mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika Mkoa wa Morogoro Bw. Keneth Shemdoe amebainisha changamoto za kiutendaji za idara ya ushirika kama uhaba wa watumishi ngazi ya Mkoa na Halmashauri zake kuwa na idadi ndogo ya wanachama kulinganisha na idadi ya wakulima na baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika kutokuwa waaminifu hali inayopelekea kutokea kwa migogoro yaara kwa mara.
Mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika Mkoa wa Morogoro Bw. Keneth Shemdoe akisoma taarifa ya ushirika wakati wa kufunga jukwaa la ushirika Juni 21 mwaka huu.
Aidha Bw. Shemdoe ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kuendelea kuchukua hatua na kutatua changamoto za ushirika hapa nchini kupitia ofisi ya mrajisi wa Mkoa kwa kuimarisha udhibiti wa misingi ya utawala bora na uwajibikaji wa vyama vya ushirika kwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara na kutatua migogoro kwa kutoa ushauri wa kisheria kwa vyama hivyo.
Akisoma risala kwa Mgeni rasmi, mwenyekiti wa Jukwaa la Maendeleo ya vyama vya Ushirika Mkoa wa Morogoro Iddy Bilali pamoja na kueleza mafanikio yaliyopo katika jukwaa hilo, ameeleza changamoto wanazokumbana nazo zikiwemo za wanachama wa vyama vya ushirika kutorejesha mikopo kwa wakati, kukosekana kwa viwanda vya kusindika mazao pamoja wanunuzi kununua mazao ya wakulima kwa bei ndogo na kwenda kuyauza kwa bei ya juu hali inachangia kurudisha nyuma utendaji.
Mwenyekiti wa jukwaa la usirika Mkoa wa Morogoro Bw. Iddy Bilali akisoma risala ya jukwaa hilo mbele ya mgeni rasmi wakati wa kufunga kwa jukwaa hilo Juni 21 mwaka huu katika ukumbi wa Savoy Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Maafisa ushirika kutoka Halmashauri za Mkoa wa Morogoro wakiwa katika mkutano wa jukwaa la ushirika lililofanyika Juni 21 mwaka huu katika ukumbi wa Savoy Manispaa ya Morogoro.
Naye Bw. Philipo Mruto ambaye ni mwakilishi wa AMANI AMCOS na Mmiliki wa Mruto Solution ameshauri wakulima kushirikiana na vyama mbalimbali vya ushirika ili kuweza kupata masoko ya uhakika na bei zenye kuridhisha, kwani kuwa nje ya vyama hivyo ni kuruhusu utapeli na kuumiza wakulima kupitia bei ndogo za mazao.
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Mhe. Pascal Kihanga akiwa picha ya pamoja na baadhi ya maafisa ushirika wa Mkoa wa Morogoro (wa tatu kushoto ni Mrajisi wa Mkoa huo Bw. Keneth Shemdoe).
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.