Wakulima wa miwa katika Bonde la Kilombero Mkoani Morogoro wamenufaika kwa kiasi kikubwa na mfumo wa upangaji wa vyama vya ushirika kikanda hivyo kuongeza tija ya uzalishaji wa zao hilo na kuwainua wakulima hao kiuchumi.
Hayo yamebainishwa Aprili 25 mwaka huu na Bw. Collins Nyakunga kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwassa kwenye hafla ya ugawaji wa mali na madeni kwa AMCOS za miwa bonde la kilombero baada ya kupangwa kikanda, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Community Centre uliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero Mkoani humo.
Bw. Collins ambaye ni Naibu Mrajisi wa Vyama vya Ushirika kutoka Tume ya Maendeleo Ushirika (TCDC) amesema kabla ya kuvigawa vyama hivyo kikanda kulikuwa na changamoto nyingi kwenye uendeshaji na usimamizi wa vyama vya ushirika ikiwemo kukosekana kwa uwazi wa taarifa za wanachama na ushirika, kukosekana kwa masoko ya pamoja, uvunaji wa miwa kuchukua muda mrefu, na mabenki kushindwa kuwakopesha wakulima kwa kuhofia kuwa fedha zitakazokopeshwa kutorudishwa kwa wakati.
“… kuwapanga wakulima kijiografia kumesaidia kuleta uwazi wa uendeshaji wa shughuli za kila siku za ushirika, imesogeza karibu shughuli za uvunaji wa miwa, vile vile kuongeza taasisi za kifedha na ujasili wa kukopesha…” amesema Bw. Collins.
Aidha, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuongeza Bajeti ya Sekta ya Kilimo kutoka Tsh. Billion 200 hadi Tsh. Billion 900 kwa mwaka wa fedha 2023/24 hivyo kuwafanya wakulima kuongeza tija ya uzalishaji na kujiinua kiuchumi.
Sambamba na hilo Bw. Collins amewataka wakulima kuendelea kujiunga na vyama vya ushirika ili kuendelea kupata mafanikio, pia amesisitiza vyama hivyo kutumia mfumo wa kielektroniki kwenye usimamizi na uendeshaji wa shughuli za vyama vyao.
Kwa upande wake Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Morogoro Bw. Kenneth Shemdoe ameeleza lengo la mkutano huo kuwa ni kugawa mali na madeni ya vyama vya ushirika 7 ambavyo vimefutwa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika baada ya zoezi la upangaji wa vyama hivyo kikanda kukamilika.
Amesema Bonde la Kilombero lilikuwa na vyama vya Ushirika 20 ambavyo vilikuwa na changamoto kadhaa hususan kwenye uvunaji wa miwa kupeleka kiwandani, lakini amesema baada ya upangaji wa kikanda kukamilika kwa sasa vipo vyama 17 ambavyo vinatambulika na Tume ya Maendeleo ya Ushirika.
Nae Mwakilishi wa wakulima wa vyama vya ushirika kutoka Halmashauri za Ifakara na Kilosa Bw. James Charles Ameishukuru Serikali kwa kushirikiana na viongozi wa kiwanda cha sukari kupanua kiwanda hicho hivyo changamoto ya upatikanaji wa soko la uhakika kwa sasa itakuwa historia ambapo kwa sasa watazalisha miwa kwa wingi na kupeleka kiwandani kwa wakati.
Aidha, ameongeza kuwa Serikali imewezesha upatikanaji wa pembejeo za kilimo bei nafuu hivyo kuendelea kuongeza uzalishaji wenye tija.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.