Vyama vya Ushirika hapa nchini vimetakiwa kufuata mwongozo wa mfumo mpya wa elektroniki wa usimamizi wa vyama vya ushirika pamoja na Waraka wa Mrajisi Na.2 wa mwaka 2022 ili kuleta ufanisi katika usimamizi wa vyama hivyo.
Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ally Mussa akiongea na viongozi na wanachama wa vyama vya ushirika wakati akifungua mafunzo ya mfumo mpya wa kielektroniki ambao utatumika kusimamia na kuendesha shughuli za vyama vya ushirika.
Hayo yameelezwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa Disemba 7 mwaka huu wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya mfumo wa kielektroniki wa usimamizi wa vyama vya Ushirika kwa Maafisa Ushirika wa Mikoa ya Morogoro na Pwani yaliyoandaliwa na Tume ya maendeleo ya Ushirika ambayo yamefanyika katika Hoteli ya Savoy Manispaa ya Morogoro.
Mrajisi Msaidizi Mkoa wa Pwani akipokea Kompyuta kutoka kwa mgeni rasmi Dkt. Mussa Ally Mussa, kompyuta hizo zimetolea na Tume ya maendeleo ya Vyama vya Ushirika kwa ajili ya kusimamia shughuli za vyama kwa mfumo wa kielektroniki.
Mrajisi Msaidizi wa vyama vya ushirika Mkoa wa Morogoro Bw. Kenneth Shemdoe akipokea kompyuta kwa ajili ya shughuli za vyama vya ushirika kupitia mfumo mpya wa kielektroniki.
Dkt. Mussa Ali Mussa ametaja faida za matumizi ya mfumo huo wa kielektroniki kuwa ni pamoja na kuongoza vyama vya ushirika katika uboreshaji na utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Serikali kwenye ushirika, kuboresha usimamizi na uendeshaji wa vyama hivyo vya ushirika, kuwezesha upatikanaji wa masoko kwa wakulima, pamoja na kuinua uchumi wa wanaushiriki na Uchumi wa Taifa kwa jumla.
“...kwa vyama vyote vya ushirika kuzingatia mwongozo wa mfumo wa usimamizi wa vyama vya ushirika pamoja na waraka wa mrajisi namba mbili (2) wa mwaka 2022... aidha kila chama kuhakikisha kinakuwa na vifaa vya tehama..” Amesema Dkt. Mussa Ali Mussa.
Katibu Tawala huyo amesema vyama hivyo vimekuwa vikikabiliwa na changamoto mbalimbali zilizopelekea baadhi yao kuteteleka ama kufa kabisa kutokana na changamoto hizo zikiwemo za ugumu wa kuhuisha daftari la taarifa za usajiri wa vyama vya ushirika na wanachama wa ushirika, utendaji usioridhisha, ukosefu wa taarifa sahihi na uwepo wa mifumo duni ya mawasiliano.
Sambamba na hilo Katibu Tawala huyo amesema Serikali inatambua kuwa vyama vya ushirika ni silaha ya wanyonge na nguzo kuu ya ujenzi wa uchumi jumuishi wa Taifa katika kufikia malengo na mipango ya maendeleo ili kuwafikia wananchi wengi, kwa mantiki hiyo, ikaamua kutunga sheria ya vyama vya ushirika namba sita (6) ya mwaka 2013 kwa lengo la kusimamia na kuratibu maenedeleo ya vyama vya ushirika hapa nchini.
Baadhi ya wataalam viongozi na wanachama wa vyama vya ushirika wakimsikiliza mgeni rasmi Dkt. Mussa Ali Mussa akitoa hotuba yake ya ufunguzi wa mafunzo ya mfumo wa elektroniki.
Kwa upande wake Bw. Kenneth Shemdoe ambaye ni Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Morogoro amesema lengo la kuwepo kwa mafunzo hayo kwa maafisa wa ushirika kutoka mikoa ya Pwani na Morogoro ni kuongeza ufanisi katika kusimamia na kuendesha majukumu ya vyama vya ushirika kwa kupitia mfumo huo mpya wa kielektroniki.
Bw. Kenneth Shemdoe ametoa wito kwa wananchi wa Mikoa hiyo miwili kujiunga na vyama vya Ushirika kwa kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ipo macho na vyama vya ushirika na kwamba usimamizi wake unatakiwa uwe wa hali ya juu wanachama wake wasidhurumiwe kwa aina yoyote.
Bw. Kenneth Shemdoe akielezea lengo na umuhimu wa mafunzo hayo kwa maafisa ushirika katika Mkoa wa Morogoro.
Nae Bw. Beatus Ligogoderi ambaye ni Mhasibu wa chama cha Ushirika cha Ulanga – Kilombero amesema mafunzo hayo yatawasaidia wanaushirika katika kutunza kumbukumbu na mali za ushirika pamoja na kuwasaidia wakulima kupata masoko ya uhakika.
Kwa upande wake Bw. Karunda Mfumo huo utasaidia kuongeza mnyororo wa thamani kwenye kilimo kwa sababu mfumo utaleta taarifa sahihi hususani upatikanaji wa masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi hivyo wakulima watakuza kipato chao.
Picha za mgeni rasmi akiwa kwenye picha ya pamoja na Maafisa, Viongozi, na wanachama wa vyama vya ushirika kutoka mikoa ya Morogoro na Pwani baada ya ufunguzi wa mafunzo ya mfumo mpya wa kielektroniki kwa ajili ya vyama vya ushirika.
Mafunzo hayo ya siku tatu kwa mikoa ya Morogoro na pwani ni mwendelezo wa mafunzo yaliyoanza mwezi Januari mwaka huu na hadi sasa yametolewa kwa Maafisa Ushirika wa kutoka mikoa 19 sasa huku yakitarajiwa kuhitimishwa Disemba 31 mwaka huu.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.