Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amewataka waajiri Mkoa wa Morogoro kuendelea kutatua changamoto za wafanya kazi wao ili kuleta chachu mahari pa kazi kwa maslahi mapana ya wafanyakazi wenyewe, wanamorogoro na Taifa kwa ujumla.
Wito huo umetolewa leo Mei 1, 2025 wakati wa maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani yenye kaulimbiu inayosema "Uchaguzi Mkuu 2025, Utuletee viongozi wanaojali haki na maslahi ya wafanyakazi, wafanyakazi tushiriki" Maadhimisho hayo yamefanyika uwanja wa Jamhuri uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Mhe. Malima amesema kuna umuhimu wa waajiri kuwajali na kuwathamini wafanyakazi kwa kuwatatulia changamoto wanazokumbana nazo ili kuweza kuwapa motisha ya kufanya kazi kwa bidii na kuiletea kampuni husika maendeleo inayoyatarajia.
".. Nichukue fursa hii kuwaelekeza waajiri wote wa Sekta binafsi katika Mkoa wa Morogoro kutatua changamoto za wafanyakazi wao.." Amesisitiza Mhe. Adam Malima
Aidha, kiongozi huyo ameitaka Ofisi ya Afisa kazi Mkoa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye maeneo ya kazi ili kujiridhisha kama mikataba ya wafanya kazi inazingatia sheria za kazi na kubaini wanaovunja sheria.
Sambamba na hayo Mkuu huyo wa Mkoa amewataka viongozi wa OSHA Mkoani humo kuhakikisha wanashughulikia malalamiko ya wafanya kazi na kuwachukulia hatua za kisheria waajiri wote wanaokiuka misingi ya kisheria na kukomesha baadhi ya tabia za baadhi ya waajiri kukiuka na kuwakandamiza wafanyakazi.
Kwa upande wa maslahi ya watumishi Mhe. Malima amesema Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuboresha maslahi yao kwa kuwaongezea mishahara na kuendelea kutoa ajira na kupunguza changqmoto ya upungufu wa watumishi ambapo mwaka 2023/2024 watumishi 741 waliajiriwa katika Halmashauri za Mkoa wa Morogoro na mwaka 2024/2025 jumla ya wafanya kazi 1491 wameajiriwa.
Kwa upande wa wafanyakazi kupitia risala iliyosomwa mbele ya mgeni rasmi, wameiomba Serikali kushughulikia changamoto zikiwemo madai mbalimbali ya wafanyakazi yakiwemo yanayohusu likizo, uhamisho, matibabu, kukaimu, kujikimu, stahiki za ajira mpya, malimbikizo ya mishahara kwa waliondolewa kazini kimakosa mwaka 2017 pamoja na malipo ya mafao ili kuhakikisha watumishi wanapata stahiki zao kwa mujibu wa sheria.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.