Naibu Katubu Mkuu Ofisi ya Rais - TAMISEMI Dkt. Charles Msonde akitoa hotuba ya kufunga mafunzo endelevu ya Walimu shuleni.
Kutokana na ongezeko la vitendo vya ukatili na unyanyasaji dhidi ya watoto hapa nchini, maafisa elimu wameagizwa kusimamia kwa karibu usalama wa wanafunzi ndani na nje ya shule kwa lengo la kuwasaidia kutimiza ndoto zao.
Agizo hilo limetolewa Januari 28 mwaka huu na Dkt. Charles Msonde Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI anayeshughulikia Elimu, kwenye hafla ya kuhitimisha Semina ya Mafunzo Endelevu ya Walimu shuleni (MEWAKA) iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano uliopo katika Chuo Cha Uwalimu Morogoro.
Dkt. Msonde amesema kuwa jambo la ukatili kwa watoto halikubaliki kutokana na uwepo wa matukio mengi ya ukatili na unyanyasaji hadi kwenye familia, jamii na shuleni hivyo walimu wanatakiwa kujiepusha na ukatili.
Aidha, Naibu Katibu Mkuu huyo amesisitiza kuwa adhabu zitolewe kwa mujibu wa sheria hivyo wanatakiwa kuzingatia sheria hizo za utoaji wa adhabu kwa wanafunzi.
Washiriki wa mafunzo ya MEWAKA wakimsikiliza mgeni rasmi akitoa hotuba yake ya kuhitimisha mafunzo ya MEWAKA.
“... na jambo hili la ukatili halikubaliki kwa watoto, jambo hili linaonekana sio tu shuleni, linaonekana lipo kwenye jamii, linaonekana lipo nyumbani... tuzuie na kukataa ukatili wa watoto”. Amesema Dkt. Msonde.
Kwa upande wake Afisa Elimu Mkoa wa Songwe ambaye pia ni Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Elimu Mkoani humo Bwana Michael Ligola amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuipa kipaumbele sekta ya elimu Kwa kuhakikisha sekta hiyo ina imarika.
Afisa Elimu Mkoa wa Songwe ambaye pia ni Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Elimu Bwana Michael Ligola akitoa neno la shukrani kwa mgeni rasmi baada ya kuhitimishwa kwa Mafunzo Endelevu kwa Walimu kazini.
Aidha, Afisa Elimu huyo amemthibitishia mgeni rasmi kuwa lengo la mafunzo hayo ni kwenda kufanya mageuzi katika sekta ya elimu na kuhakikisha ujuzi walioupata unakuwa na matokeo.
Sambamba na hilo, Bw. Ligola kwa niaba ya walimu wenzake waliopata mafunzo ya MEWAKA kupitia semina hiyo ya siku mbili amemuomba Naibu Katibu Mkuu huyo wa TAMISEMI kuwa na kikao cha tathmini ya mafunzo hayo ili kujua kama kile walichojifunza ndicho wanachokifanyia kazi katika maeneo yao pamoja na kutatua kwa pamoja changamoto zitakazokuwa zimejitokeza kwa kipindi hicho kifupi.
Mgeni rasmi Dkt. Charles Msonde akiwa kwenye picha ya pamoja na Maafisa Elimu wa Mikoa, Halmashauri na Waratibu wa Mafunzo ya MEWAKA mara baada ya kuhitimishwa kwa mafunzo hayo.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.