.Wananchi wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mikumi Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro wamekubaliana kujenga Shule mpya tatu za Sekondari zitakazoanza kutumika mwakani ili kupunguza msongamano wa wanafunzi katika Shule ya Sekondari ya Mikumi ambayo ndiyo shule pekee katika Mji huo.
Makubaliano hayo yamefikiwa hivi karibuni na wananchi wa Kata ya Mikumi walipotembelewa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare wakati wa ziara ya kikazi katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mikumi ambapo alifanya kikao na wananchi wa kata hiyo kwa ajili ya kuweka mikakati ya ujenzi wa Shule hizo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao akiwemo Gladness Lukumayi Mkazi wa Mikumi kijiji cha Ihombwe amesema hatua hiyo ya kutaka kuenga shule mpya inatokana na wanafunzi walio wengi kutembea umbali mrefu kutoka wanakoishi hadi Shule ya Sekondari ya Mikumi hivyo kupelekea wanafunzi wengi kupata changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na wanafunzi wa kike kupata mimba na kupoteza haki zao za kupata Elimu.
Naye Elius Edward Mkazi wa kijiji cha Msimba amesema changamoto wanazokumbana nazo wazazi katika kuwasomesha wanafunzi hao ndio zinazopelekea wananchi kuwa na hamasa ya kujenga Shule katika kijiji chao ili kuepukana na gharama za usafiri wa kila siku.
Akizungumza katika kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare ametoa pongezi kwa wananchi wa Mji huo kwa kufikia muafaka wa ujenzi wa Shule za Sekondari tatu kisha kuwataka wananchi hao kuchangia michango ya ujenzi wa Shule hizo ili kuweza kuepukana na changamoto mbalimbali walizozitaa ikiwa ni pamoa na wanafunzi kukaa katika vyumba vya kupanga maarufu kama mageto.
Loata Sanare amebainisha kuwa zaidi ya wanafunzi 1120 Mkoani humo wamesitisha masomo katika kipindi cha miaka minne huku Mamlaka ya Mji Mdogo Mikumi ikiongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wa kike kupata mimba wakiwa hawaamaliza masomo yao.
Aidha, Loata Sanare amesema sababu ambazo zimechangia idadi kubwa ya wanafunzi kutoendelea na masomo ni kupata mimba na kutembea umbali mrefu ili kufika Shule ya Sekondari Mikumi ambapo wanafunzi hulazimika kutembea zaidi ya kulometa 30 kila siku kufika Shuleni hapo.
Sambamba na hayo Loata Sanare amekerwa na kitendo cha wanafuzi kukaa katika nyumba za kupanga (GHETTO) akibainisha kuwa ndiyo sababu inayopelekea wanafunzi kupata mimba kutokaka na kutokuwepo uangalizi wa karibu wa wazazi ama walezi kwa wanafunzi hao.
‘’Mtoto anakaa ghetto unajuaje usalama wake, wazazi mnakuwa na amani na kulala salama, mzazi wa hapa mtoto wako wa kike hata wa kiume siku hizi yupo getto hana mzazi ambaye umemuachia umeenda ukampangishia chumba ukamwambia mtoto kaa hapa, ikifika saa moja naye anaenda kufanya shughuli zake’’ amesema Sanare
Katika hatua nyingine Loata Sanare amewataka watendaji wa vijiji kuwahamasisha wananchi kwa ajili ya ujenzi wa shule hizo huku akitoa onyo kali la kuwachukulia hatua za kisheria mwanacnhi ambaye atapingana na agizo hilo la uchanga fedha kwa aili ya maendeleo ya shule mpya zitakazojengwa katika hapo Mikumi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.