Wandishi Morogoro wahimizwa kutoa elimu kwa jamii.
Shirika la Childhood Development Organization (CDO) limetoa mafunzo kwa Waandishi wa habari Mkoa wa Morogoro kuhusu Sayansi ya Malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto ili kuwa na uelewa na kuweza kupeleka elimu hiyo katika jamii zinazowazunguka.
Mafunzo hayo kwa waandishi wa habari yametolewa Februari 16, 2024 na Mratibu wa Shirika la CDO Bw. Innocent Rusumyo kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.
Bw. Innocent amesema kuwa Shirika hilo limepewa dhamana na Serikali kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro pamoja na wadau kuratibu utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT – MMMAM) Mkoani humo.
Aidha, ameeleza kuwa kupitia Mradi wa Mtoto Kwanza ambao unalenga kusukuma utekelezaji wa program hiyo ngazi ya mikoa hushirikisha Waandishi wa Habari kama wadau muhimu katika kuripoti, na kuibua ajenda zinazohusu masuala ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto katika jamii, hivyo wametoa mafunzo hayo kwa waandishi hao ili waweze kuipeleka elimu hiyo kwenye jamii.
“...Baada ya mafunzo haya jamii zetu hasa za Mkoa wa Morogoro ambao zinasikiliza vyombo mbalimbali vya habari wanaweza kupata uelewa juu ya kumlea mtoto akiwa na umri wa mwaka sifuri hadi miaka nane….” Amesema Bw. Innocent.
Katika hatua nyingine, Mratibu huyo amebainisha kuwa tafiti zinaonesha kuwa asilimia 43 ya watoto wa miaka sifuri hadi miaka nane wapo katika hatari ya kutofikia ukuaji timulifu, hivyo Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuanzisha program hiyo ambayo inagusa maeneo matano ambayo ni lishe bora, Afya, ujifunzaji wa awali, ulinzi na usalama pamoja na malezi yenye muitikio.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika hilo Bi. Felistas Kalomo amewahimiza wanaume Mkoani humo kuacha tabia ya kuwatelekeza wanawake pindi wanapokuwa wajawazito na kuwataka kushirikiana katika kipindi cha ujauzito na pale mwanamke anapojifungu.
Naye mwakilishi wa Waandishi wa habari waliopata mafunzo hayo Mwajuma Rambo amesema watakuwa bega kwa bega katika kufikisha elimu kwa jamii inayowazunguka ya namna bora ya malezi na makuzi kwa watoto na kwa jinsi gani wazazi wanatakiwa kulea watoto ili waweze kukua katika afya iliyo bora.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.