WAANDISHI MOROGORO WATAKIWA KUANDIKA HABARI ZENYE TIJA KWA JAMII.
Waandishi wa habari Mkoani Morogoro wametakiwa kuandika na kutoa habari zinazohusu maendeleo na kwa kuzingatia kanuni, taratibu na maadili ya tasnia yao badala ya kuandika habari zinazoweza kuleta taharuki kwa jamii hivyo kuondoa taswira nzuri ya Mkoa huo.
Kaimu Katibu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Rosalia Rwegasira akifungua Kikao cha waandishi wa habari na wadau wa habari kutoka vyombo vya ulinzi na usalama Mkoani humo Juni8 Mwaka huu.
Hayo yamebainishwa Juni 8 mwaka huu na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Rosalia Rwegasira wakati akifungua kikao kazi kilichowahusisha waandishi wa habari na wadau wa habari kutoka vyombo vya Ulinzi na Usalama Mkoani humo, ambacho kimefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Dkt.Rosaria amesema Waandishi wa habari kupitia kalamu zao wana nguvu katika kubadilisha mwelekeo wa Jamii kuwa hasi au chanya kwa msingi huo amewataka kutumia vema kalamu zao kufikisha taarifa sahihi kwa jamii ili kuepuka kuleta taharuki kwa jamii kupitia taarifa zisizokuwa za uhakika na kuhakikiwa na pande mbili zinazohusika.
Aidha Dkt. Rosalia ameongeza kuwa Serikali ya Mkoa wa Morogoro ina miradi mingi ya maendeleo na ya kimkakati ambayo ni ya muda mrefu na muda mfupi, iliyokamilika na inayotarajiwa kukamilika ambayo mwananchi ana haki ya kufahamishwa, kazi inayotakiwa kufanywa na waandishi wa habari kama mchango wao katika kuinua Mkoa wa Morogoro.
“Ningependa kuona kwamba, kama ambavyo mnazitoa kwa sasa pia muendelee kutoa zaidi taarifa zinazohusu maendeleo ya Mkoa wetu wa Morogoro, kwani Mkoa wetu una fursa nyingi za Miradi ya Kimaendeleo” amesema Dkt. Rosalia.
Baadhi ya wanachama wa Morogoro Press Club wakishiriki kikao kazi cha majadiliano baina ya waandishi wa habari na wadau kutoka vyombo ya ulinzi na usalama Mkoani MorogoroJuni 8 Mwaka huu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Morogoro (Morogoro Press Club) Bw. Nickson Mkilanya amesema kikao hicho ni muendelezo wa mpango mkakati wa kuboresha mahusiano ya kikazi baina ya waandishi wa habari na wadau wa vyombo vya Ulinzi na Usalama lengo likiwa ni kuboresha utendaji kazi wa pande hizo mbili.
Naye mwandishi wa habari wa ITV Idda Mushi kwa niaba ya waandishi wenzake amewataka kuendelea kuheshimu misingi, kanuni, taratibu na maadili ya tasinia ya Habarai pamoja kuzingatia na kutekeleza sheria za nchi muda wawapo katika majukumu yao ili kuliweka Taifa la Tanzania katika sehemu salama kwa kutoa taarifa sahihi na zinazolenga ustawi wa jamii.
Sambamba na hayo Mwakilishi wa Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Morogoro Bw. Christopher Mwakajinga ameweka wazi kuwa TAKUKURU wapo tayari kuendeleza mahusiano na Chama cha Morogoro Press Club pamoja na waandishi wote Mkoani na kuahidi kuwa TAKUKURU Mkoani humo itaandaa semina ya waandishi hao kwa ajili ya kuwapa mafunzo maalum ya kupata uelewa na majukumu ya taasisi hiyo ili waweze kuifahamisha jamii.
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro akiwa katika picha ya pamoja na Chama cha waandishi wa habari pamoja na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama Mkoani humo baada ufunguzi wa kikao hicho Juni 8 Mwaka huu.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.